Jun 09, 2020 08:02 UTC
  • Muqtada al-Sadr: Marekani inapaswa kuondoa vikosi vyake vyote Iraq

Kiongozi wa Harakati ya Al-Sadr ya nchini Iraq ameitaka Marekani iviondoe mara moja vikosi vyake vyote katika ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Sayyid Muqtada al-Sadr ametoa mwito huo katika taarifa ya usiku wa kuamkia leo ambapo amesisitiza kuwa, "Washington imekuwa ikitaka kila mtu aipigie magoti kupitia njia zake za kigaidi kama kuchochea vita, mauaji, vitisho, sambamba na kutaka kupanua satua yake kote duniani."

Amesema kuna udharura kwa Marekani kubadilisha mienendo yake ya kiuhasama dhidi ya raia wake wenyewe na dhidi ya dunia na iwarejeshe nyumbani wanajeshi wake vamizi walioko katika nchi mbalimbali duniani hususan Iraq.

Sayyid Sadr ameeleza bayana kuwa,  lengo hasa la Washington kusalia nchini Iraq ni kulifanya taifa hilo lisalimu amri mbele ya Marekani na wala si kuikomboa nchi hiyo kutoka katika mikono na uvamizi wa kundi la kigaidi la Daesh, 

Askari vamizi wa US nchini Iraq

Mwanzoni mwaka huu pia, mwanazuoni huyo maarufu wa Iraq alitoa ujumbe kwenda kwa spika wa bunge la nchi hiyo akitaka kupigwa kufuli ubalozi wa Marekani na kambi zake za kijeshi nchini humo.

Licha ya jeshi la Iraq kutangaza habari ya kutamatisha operesheni dhidi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) tangu mwanzoni mwa mwaka 2018, lakini muungano wa kijeshi wa Marekani unaendelea kutafuta vijisababu vya kusalia katika nchi hiyo ya Kiarabu yenye utajiri wa mafuta.

Tags