Amnesty International: Saudia iache kuwatesa wanaharakati wanawake iliowaweka korokoroni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i61822-amnesty_international_saudia_iache_kuwatesa_wanaharakati_wanawake_iliowaweka_korokoroni
Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International limeitaka Saudi Arabia iache utesaji na ukiukaji mkubwa inaofanya wa haki za wanaharakati wanawake wanaoshikiliwa kwenye jela za nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 25, 2020 22:00 UTC
  • Amnesty International: Saudia iache kuwatesa wanaharakati wanawake iliowaweka korokoroni

Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International limeitaka Saudi Arabia iache utesaji na ukiukaji mkubwa inaofanya wa haki za wanaharakati wanawake wanaoshikiliwa kwenye jela za nchi hiyo.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesisitiza katika taarifa liliyotoa juu ya kuachiliwa huru bila masharti yoyote wanaharakati wa kike wanaoshikiliwa kwenye magereza ya Saudia.

Amnesty International imebainisha kuwa, idadi kadhaa miongoni mwa wanaharakati hao wanawake wameteswa na kudhalilishwa kingono au kuwekwa kwa muda mrefu katika seli ya mtu peke yake.

Kwa mujibu wa shirika hilo la Msamaha Duniani, mageuzi yanayodaiwa kufanywa na viongozi wa Saudia hayawezi kuwa ni kisingizio cha kufunika ukiukaji wa haki za binadamu na ukandamizaji wa kinyama wanaofanyiwa wanaharakati wa haki za binadamu.

Mrithi wa ufalme wa Saudia, Mohammad bin Salma (kulia) anayetumia kisingizio cha mageuzi kukandamiza haki za raia wa nchi hiyo

Mwezi Mei mwaka 2018, vikosi vya usalama vya Saudi Arabia viliwatia nguvuni wanaharakati kadhaa wanawake kwa sababu ya kupigania haki sawa za kiraia kati ya wanawake na wanaume nchini humo.

Mashirika na asasi nyingi za kimataifa na za kutetea haki za binadamu, likiwemo Shirika la Human Rights Watch, hadi sasa zimeshatoa taarifa mara kadhaa za kukosoa ukandamizaji wa haki ya utoaji maoni, kunyongwa na kuwekwa korokoroni wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Saudia.

Kwa mujibu wa mashirika na asasi hizo, utawala wa Aal Saudi ni miongoni mwa wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu duniani.../