Waandishi 40 wafukuzwa kazi kwa kumkosoa waziri mkuu wa Israel
-
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu
Udikteta na ukosefu wa uhuru wa waandishi wa habari umezidi kujidhihirisha ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya waandishi 40 wa habari kufutwa kazi kwa kumkosoa waziri mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu.
Gazeti la Yedioth Ahronoth limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Barak Ravid, mwandishi wa habari wa utawala wa Kizayuni wa habari za kidiplomasia pamoja na waandishi wengine 39 jana Jumapili walipokea barua za kuachishwa kazi na taasisi zao kutokana na kumkosoa waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu na masuala mengine ya kisiasa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kabla ya hapo Netanyahu aliwahi kumlalamikia vikali Barak Ravid na waandishi wengine kwa kumkosoa.
Ikumbukwe kuwa hivi sasa waziri mkuu huyo wa Israel ana kesi nne za ufisadi anatakiwa kuzijibu mahakamani. Ilikuwa imepangwa kuwa kesi za Netanyahu zisikilizwe mwezi Machi mwaka huu lakini ziliakhirishwa kutokana na maambukizi ya kirusi cha corona.
Kesi za ufisadi ni moja ya sababu kuu za upinzani wa makundi ya kisiasa ya Israel kwa waziri mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu.
Huku hayo yakiripotiwa, usiku wa kuamkia leo utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya mashambulizi mengine ya anga katika Ukanda wa Ghaza.
Televisheni ya al Mayadeen imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, ndege za utawala wa Kizayuni zimeshambulia eneo la al Zaitun, mashariki mwa Ukanda wa Ghaza.
Hadi tunapokea habari hii kulikuwa hakujatangazwa hasara zozote zilizosababishwa na mashambulio hayo ya kikatili ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza uliozingiwa kila upande.