Abdul-Salaam: Wanachotaka wavamizi sio amani ni kusalimu amri Yemen
Mkuu wa timu ya mazungumzo ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen ametangaza kuwa, unachotaka muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia huko Yemen sio amani bali ni kusalimu amri Yemen.
Muuhammad Abdul-Salaam ambaye pia ni msemaji wa Harakati ya Wananchi ya Ansarullah ameeleza kuwa, mataifa yanayounda muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia na Umoja wa Mataifa hayatoi mapendekezo yenye kuleta ushirikiano chanya, na hilo linatokana na kuwa, wanachotaka wao sio amani bali ni kuona Yemen inasalimu amri.
Aidha amesema kuwa, wananchi wa Yemen wataubadilisha mzingiro wa wavamizi dhidi yao na kuwa fursa kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa kijeshi na kiulinzi wa nchi hiyo.
Mkuu wa timu ya mazungumzo ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen ameukosoa pia utendaji wa Umoja wa Mataifa na kueleza kuwa, tangu taasisi hiyo ilipoasisiwa imekuwa chini ya udhibiti wa Marekani na Uingereza.
Hivi karibuni mkuu huyo wa timu ya mazungumzo ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa nchini Yemen alisema kuwa madai yanayotolewa na serikali ya Saudi Arabia kwamba inataka kuwepo amani nchini Yemen ni uongo mtupu.
Saudi Arabia ikipata himaya na uungaji mkono wa Marekani, Uingereza, Imarati na nchi nyingine kadhaa, ilianza kuishambulia kijeshi Yemen Machi 2015 na kuizingira nchi hiyo baharini, angani na nchi kavu. Kinyume na matarajio yao, hadi sasa watawala wa Aal Saud wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen.