Palestina yaitaka ICC ifanye uchunguzi kuhusu jinai za Israel
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) ichukue hatua za haraka za kuchunguza jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel hasa kitendo cha utawala huo cha kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesema uchunguzi huo unapaswa kuanzishwa haraka ili maafisa watenda jinai wa Israel waweze kuadhibiwa. Wizara ya Mambo ya Nje ya Paletina imelaani kitendo cha wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel cha kuafiki ujenzi wa vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni katika eneo la Mashariki la Al-Issawiya mashariki mwa mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu. Taarifa hiyo imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka za kusitisha upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imetahadharisha kuwa, uamuzi mpya wa utawala wa Kizayuni wa kuendelea na hatua zake za kivamizi dhidi ya Quds Tukufu na wakaazi wa mji huo unatekelezwa kwa lengo la kubadilisha ukweli wa mambo wa mji huo pamoja na historia na utambulisho wake.
Utawala wa Kizayuni wa Israel, ambao unapata himaya kamili ya Marekani, umekiuka azimio 2334 la Baraza la Usalama, ambalo Disemba 2016 lilitaka ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni usitishwe.