Makumi ya waitifaki wa Saudia waangamizwa katika shambulio mkoani Maʼrib
Mlipuko uliotokea katika mkoa wa Maʼrib huko katikati mwa Yemen umeangamiza makumi ya mamluki na waitifaki wa Saudi Arabia.
Ripoti zinasema kuwa, makumi ya mamluki wa chama cha Islah na vinara wa makabila yenye mfungamano na Saudi Arabia inayoendelea kushambulia maeneo mbalimbali ya Yemen na kuua raia wasio na hatia, wameuawa katika mlipuko huo uliotokea kwenye kikao cha mamluki hao eneo la Matarih Najlaa, katika mkoa wa Maʼrib.
Makumi ya mamluki wengine wamejeruhiwa katika kikao hicho kilichojumuisha watu mashuhuri wa eneo hilo na viongozi wa chma cha Islah.
Hadi sasa sababu ya mlipuko huo bado haijajulikana lakini baadhi ya duru zinasema kuwa, ulikuwa shambulizi la kombora la jeshi la Yemen na wapiganaji wa harakati ya Ansarullah.
Mauaji hayo yamefuatia mashambulizi ya siku kadhaa ya mizinga na ndege za kivita za Saudi Arabia na washirika wake ambayo yamekiuka mapatano ya kusitisha vita.
Mkoa wa Maʼrib una umuhimu mkubwa wa kiuchumi kwa nchi ya Yemen kutokana na kuwa na vyanzo vya mafuta na gesi, bwawa kubwa la Maʼrib na kilimo cha umwagiliaji.