Wanajeshi 11 wa Yemen waachiliwa huru
Mkuu wa Kamati ya Taifa ya Masuala ya Mateka wa Kivita ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen ametangaza habari ya kuachiliwa huru maafisa 11 wa jeshi waliokuwa wametekwa nyara.
Kwa mujibu wa televisheni ya al Masirah, Abdul Qadir al Murtadha alitangaza habari hiyo jana na kuongeza kuwa, mateka 11 wa jeshi la Yemen wameachiliwa huru katika operesheni ya kubadilisha wafungwa kwenye mkoa wa Maarib wa katikati mwa Yemen.
Tarehe 14 mwezi huu wa Agosti pia, mateka wanne wa jeshi la Yemen waliachiliwa huru katika operesheni ya kubadilisha wafungwa huko al Jauf.
Habari nyingine kutokana Yemen inasema kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia umefanya mashambulizi 124 katika mkoa wa al Hudaidah katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita.
Ndege za kivita za utawala vamizi wa Saudi Arabia umeendeleza mashambulizi yake ya kikatili katika maeneo mengine mbalimbali ya Yemen.
Tangu yalipotiwa saini makubaliano ya kusimamisha vita ya Stockholm mwezi Disemba 2018, pande zote zilizoshiriki kwenye makubaliano hayo ziliiahidi kusimamisha vita. Hata hivyo muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia umekataa kuheshimu angalau asilimia ndogo tu ya vipengee vya makubaliano hayo.