Serikali ya Israel yakaribia kusambaratika baada ya mizozo kuongezeka
Duru za habari kutoka Israel zinaripoti kuwa, hitilafu na mivutano katika baraza la mawaziri la utawala huo ghasibu zimeshadidi mno na kwamba, serikali hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imekaribia kusambartika.
Ripoti zaidi zinasema kuwa, hitilafu hizo zimekuwa kubwa kiasi cha kupelekea kuakhirishwa kikao cha baraza hilo la mawaziri kilichokuwa kimepangwa kufanyika leo.
Kikao hicho kimeakhirishwa baada ya kuongezeka hitilafu za kimitazamo baina ya wamawaziri kuhusiana na bajeti ya utawala huo.
Baadhi ya duru zinasema kuwa, kushadidi hitilafu hizo ni ishara ya kukaribia kusambarika serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ambayo hivi sasa inakabiliwa na matatizo chungu nzima.
Hii ni mara ya pili kuakhirishwa kwa kikao cha Baraza la Mawaziri la Israel katika kipindi cha wiki tatu zilizopita ambapo hiyo ni ishara ya wazi ya kuweko mgogoro mkubwa ndani ya baraza hilo la mawaziri.
Hayo yanajiri sambamba na kushuhudiwa mara kwa mara maelfu ya waandamanaji wenye hasira wakikusanyika mbele ya makazi ya Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel Benjamin Netanyahu yaliyopo katika mtaa wa Balfour huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) na kutaka mwanasiasa huyo ajiuzulu.
Netanyahu na baraza lake la mawaziri wanalaumiwa na waandamanaji hao wanaosema kuwa, badala ya kutanguliza mbele matatizo ya kiafya na kiuchumi yanayoisumbua Israel kwa sasa, wameng’ang’ania kusukuma mbele gurudumu la mipango ya kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.