Kushadidi maandamano Israel; kukalia kuti kavu Netanyahu na serikali yake
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i63035-kushadidi_maandamano_israel_kukalia_kuti_kavu_netanyahu_na_serikali_yake
Malalamiko na maandamano katika Israel za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepewa jina bandia la Israel yameshadidi ambapo nara za waandaanaji sasa zimekwenda mbali zaidi ambapo zinalalamikia muundo wa madaraka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 26, 2020 02:40 UTC
  • Kushadidi maandamano Israel; kukalia kuti kavu Netanyahu na serikali yake

Malalamiko na maandamano katika Israel za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepewa jina bandia la Israel yameshadidi ambapo nara za waandaanaji sasa zimekwenda mbali zaidi ambapo zinalalamikia muundo wa madaraka.

Awali waandamanaji hao walikuwa wakisisitiza kujiuzulu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, lakini sasa wamekwenda mbali zaidi na kulalamikia kile wanachokitaja kuwa muundo mbovu na usiofaa wa uongozi katika utawala huo ghasibu.

Maandamano huko Israel yamekuwa yakifanyika kwa wiki kadhaa sasa. Maandamano hayo yanafanyika kila Jumapili na kuhudhuriwa na maelfu ya watu. Kuna nara na kaulimbiu mbili kuu ambazo zimekuwa zikisikika katika mudhahara huo. Nara ya kwanza ni ile ambayo imekuwa ikipigwa dhidi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. Waandamanaji hao wanasisitiza juu ya kutokuwa na utendaji mzuri serikali yake sambamba na kesi zinazomkabili mwanasiasa huyo.

Waandamanaji wamekuwa wakibeba mabango na maberamu yenye ujumbe usemao Crime Minister yaani Waziri wa Uhalifu badala ya Prime Minister yaani Waziri Mkuu. Nara na kaulimbiu nyingine ambayo imekuwa ikisikika baina ya waandamanaji ni ya kulalamikia muundo wa uongozi ndani ya utawala huo ghasibu. Waandamanaji wamekuwa wakibeba mabango yenye maandishi “Msimu wa Machipuo Israel” mkabala na machipuo na harakati za mageuzi zilizoshuhudiwa katika nchi za Kiarabu.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu

Benjamin Netanyahu, amekuwa Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel tangu 2009. Kufanyika chaguzi tatu mtawalia katika kipindi cha mwaka mmoja na kutopata ushindi mutlaki chama chake cha Likud anachokiongoza, ni ushahidi tosha kwamba, wakazi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) hawaridhishwi na utendaji wake wa miaka 11. Hali hiyo ya kutoridhishwa inashuhudiwa zaidi katika sekta mbili muhimu za afya na uchumi.

Katika sekta ya uchumi, kushindwa serikali ya Netanyahu kukabiliana na ueneaji wa virusi vya Corona, ni moja ya sababu za maandamano na malalamiko ya maelfu ya wakazi wa Israel. Takwimu za hivi karibuni kabisa zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu 105,000 wameambukizwa virusi vya Corona huko Israel na watu 847 wameaga dunia kwa maradhi ya Covid-19.

Katika uga wauchumi, uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni unaonyesha kuwa, asilimia 62 ya washiriki wa uchunguzi huo wa maoni wameonyesha kutoridhishwa kabisa na utendaji wa Benjamin Netanyahu katika kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi. Fauka ya hayo, wakazi wa Israel wanalalamikia vikali mafaili manne ya ufisadi yanayomkabili Netanyahu na wanaamini kuwa, kutokana na satua na ushawishi alionao Waziri Mkuu huyo katika vyombo vya mahakama amekuwa akizuia kufuatiliwa kiadilifu kesi zake hizo za ufisadi.

Mgomo wauguzi Israel wakilalamikia mazingira mabaya kazini

Kwa kuzingatia hali hiyo, waaandamanaji wanaamini kuwa, Netanyahu ni Waziri Mkuu ambaye amekuwa akitumia vibaya cheo chake kwa ajili ya kufanya uhalifu. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana takwa la kujiuzulu na kuachia ngazi Benjamin Netanyahu sasa limechukua wigo mpana zaidi ambapo waandamanaji wamekuwa wakijitokeza kwa maefu kila Jumapili na kuandamana wakisisitiza kujiuzulu Benjamin Netanyahu.

Nara na kaulimbiu nyingine ambayo imekuwa ikipigwa na waandamanaji au hata kuandikwa katika mabango na maberamu wanayobeba ni Msimu wa Machipuo ya Uongozi. Waandamanaji hao wanataka kuweko mabadiliko katika mfumo wa uongozi na madaraka huko Israel. Msimu wa Machipuo ya Uongozi ulishuhudiwa katika nchi za Kiarabu 2011 ambapo wananchi wa baadhi ya mataifa walifanya maandamanao dhidi ya serikali na kupelekea kuondolewa madarakani viongozi wa nchi kama Misri, Tunisia na Libya. Hivi sasa wakazi wa Israel nao wamekuja na nara ile ile ya nchi za Kiarabu ya kutaka mageuzi kupitia kaulimbiu ya “Msimu wa Machipuo Israel Umewadia”.

Ukweli wa mambo ni kuwa, ni watu wachache sana huko Israel wanaotaka Netanyahu aendelee kuwa Waziri Mkuu wa Israel. Lakini Netanyahu ameganda na kung’ang’ania kiti hicho kiasi kwamba, hata chama chake cha Likud hakiwezi kumuuzulu.

Benny Gantz, kiongozi wa chama cha Bluu na Nyeupe ambacho ni mshirika wa Netanyahu katika serikali

Katika upande mwingine, mpasuko wa kisiasa huko Israel ni mkubwa kiasi kwamba, baraza la mawaziri la Israel linaloundwa na chama cha Likud kinachoongozwa na Netanyahu na kile cha Bluu na Nyeupe kinachoongozwa na Benny Gantz limekumbwa na mizozo na hitlafu mapema zaidi kuliko serikali zote zilizotangulia; na hivi sasa serikali hiyo ya muungano inakaribia kusambaratika.

Kwa kuzingatia hali hii, waandamanaji huko Israel ambao wanakabiliwa na mazingira mabaya ya kimaisha na wanaonekana kutaka tamaa zaidi na mustakabali wao, wameongeza kiwango cha matakwa yao ya kutaka kuachia ngazi Netanyahu kwa ajili ya kupatikana mabadiliko ya muundo wa madaraka na uongozi huko Israel.