Erdogan: Uturuki haitafumbia macho yake haki zake huko Mediterania Mashariki
Rais Recep Tayyip Erdiogan wa Uturuki ametahadharisha kuwa hatafikia mapatano yoyote katika eneo la Mediterania Mashariki na amesema kuwa, Ankara imejizatiti kuchukua hatua zozote za lazima za kulinda haki yake katika Bahari Nyeusi, Aegean na Mediterania.
Akizungumza jana Jumatano, Rais wa Uturuki ameitolea wito Ugiriki iache kufanya makosa. Rais Erdogan ameongeza kuwa, Ankara haikodolei macho ardhi, mamlaka ya kujitawala wala maslahi ya nchi nyingine. Hali ya mvutano imeongezeka kuhusu maliasili za nishati kati ya Uturuki na Ugiriki baada ya Ankara mwezi huu wa Agosti kutuma meli yake ya utafiti ijulikanayo kwa jina la Oruc Reis katika eneo linalozozaniwa la maji ya Mediterania Mashariki; hatua iliyotajwa na Athens kuwa ni kinyume cha sheria.
Wakati huo huo Nikos Dendias Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki amesema kuwa, Athens italinda kwa jina la sheria mamlaka ya ardhi na haki ya kujitawala ya nchi hiyo. Ameongeza kuwa, Ugiriki haina chaguo jingine bali kulinda mipaka yake ya kitaifa na ile ya Ulaya.
Jumanne wiki hii Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki na Ugiriki walisema kuwa wanataka kutatua mvutano baina ya nchi zao kwa njia ya mazungumzo. Hiyo ni baada ya kufanya mazungumzo na mwenzao wa Ujerumani, Heiko Maas.
Katika mzozo huu, Uturuki inasema kuwa, iko tayari kuketi kwenye meza ya mazungumzo na Ugiriki iwapo tu haki zilizopo huko Mediterania Mashariki zitagawiwa kwa uadilifu.