Hania asisitiza kuendelezwa mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesisitizia wajibu wa kuendelezwa mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni.
Akizungumza jana Ijumaa baada ya kuzuru makaburi ya mashahidi wa kambi za Sabra na Shatila katika ziara yake huko Lebanon, Ismail Hania ameeleza kuwa, damu ya mashahidi wa Sabra na Shatila ni laana ambayo itaendelea kuwafuata maghasibu na utawala wa Kizayuni na kwamba wananchi wa Palestina na Lebanon hawatamsamehe adui Mzayuni.
Hania amesema kuwa, Israel si jirani, si rafiki na wala si mshirika bali ni adui na ataendelea kuwa adui.
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesisitiza kuwa, kulipiza kisasi damu zilizomwagwa huko Sabra na Shatila kutafanyika pale tu njama hiyo ya Wazayuni katika ardhi ya Palestina itaposambaratishwa.
Kambi za Sabra na Shatila ni kambi mbili miongoni mwa kambi 12 zinazohifadhi wakimbizi wa Palestina huko kusini mwa Lebanon. Wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni walishambulia kambi mbili hizo za Sabra na Shatila kuanzia tarehe 16 hadi 18 mwezi Septemba mwaka 1982 ambazo zilikuwa zikihifadhi watu zaidi ya 20 elfu na kisha kuwauwa kwa umati wakimbizi hao wasio na hatia.
Ariel Sharon ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni na kamanda wa kijeshi wa maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu ya Lebanon alikuwa na nafasi kuu katika mauaji hayo ya umati. Jinai hizo za Wazayuni na mamluki wao dhidi ya wakazi wa kambi za Sabra na Shatila ziliendelea kwa siku tatu mtawalia na ilikadiriwa kuwa, Wapalestina 3,500 hadi 5000 waliuliwa kwa umati katika mashambulizi hayo ya kikatili ya utawala wa Kizayuni.