WHO yathibitisha Uganda haina Ebola, ugonjwa huo unaendelea kuenea Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141008-who_yathibitisha_uganda_haina_ebola_ugonjwa_huo_unaendelea_kuenea_kongo
Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha kumalizika mlipuko wa Ebola nchini Uganda.
(last modified 2026-08-27T11:59:07+00:00 )
Aug 27, 2026 11:57 UTC
  • Uganda haina tena Ebola
    Uganda haina tena Ebola

Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha kumalizika mlipuko wa Ebola nchini Uganda.

Mwezi uliopita Uganda ilitangaza rasmi kuwa haina tena maambukizi ya virusi hivyo siku 42 baada ya kuthibitishwa kuruhusiwa kutoka hospitali mgonjwa wa mwisho wa Ebola. Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliendelea kufuatilia hali hiyo ili kuhakikisha hakuna maambukizi yoyote ya virusi hivyo.

Kampala inasema kuwa maambukizo yote ya Ebola nchini humo yalisababishwa na mlipuko ulioikumba nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kwamba wagonjwa wa kwanza waliingia nchini humo wakitokea Kongo kabla ya kugundua kuwa wameambukizwa.

Mamlaka za afya Uganda zilichukua hatua za haraka kuzuia maambukizi zaidi kwa kuzuia mikusanyiko mikubwa ya watu, kuwaagiza watu kuacha kusalimiana kwa mikono na kusitisha usafiri wa umma pamoja na safari za ndege kati ya Uganda na Kongo.

Hata hivyo, hali ni tofauti sana mashariki mwa Kongo ambapo virusi vinaendelea kuenea kwa kasi inayowatia hofu maafisa wa afya. Zaidi ya visa 4,500 vimethibitishwa katika majimbo sita, vikiwemo vifo zaidi ya watu 2,000.

Mlipuko huo unasababishwa na virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo, ambayo kwa sasa haina chanjo wala matibabu yaliyoidhinishwa.

Wiki iliyopita, WHO ilisema hatari bado iko juu kwa nchi jirani, haswa zile zinazochangia mipaka ya ardhi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.