Araghchi: Mashauriano ya Beijing yamefanikiwa; Iran yathamini “ushirikiano wa kimkakati” na China
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141528-araghchi_mashauriano_ya_beijing_yamefanikiwa_iran_yathamini_ushirikiano_wa_kimkakati_na_china
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ameelezea mashauriano yake mjini Beijing kama “yaliyofanikiwa,” akizungumzia maudhui ya safari yake katika mji mkuu huo wa China, ambapo alikutana na mwenzake, Wang Yi.
(last modified 2026-09-17T12:10:19+00:00 )
Sep 17, 2026 12:09 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi
    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ameelezea mashauriano yake mjini Beijing kama “yaliyofanikiwa,” akizungumzia maudhui ya safari yake katika mji mkuu huo wa China, ambapo alikutana na mwenzake, Wang Yi.

Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X kufuatia mikutano hiyo mjini Beijing siku ya Jumatano, mwanadiplomasia huyo mkuu amesema Iran inathamini ushirikiano wake wa kimkakati wa muda mrefu na China, na kuangazia kanuni nne zilizobainishwa na Rais wa China, Xi Jinping, kama nguzo muhimu za amani ya kikanda.

Araghchi amebaini kuwa: "Iran inathamini ushirikiano wa kimkakati tulioujenga kwa muda mrefu.” Ameongeza kuwa, “Maamuzi ya leo yataamua usawa wa kimkakati wa siku zijazo katika eneo hili, kwa athari kubwa zisizopimika.”

Pia amesisitiza nafasi kubwa ya pande husika kuhusu masuala ya kikanda kwa mustakabali wa eneo hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, amegusia “kanuni nne za amani zilizobainishwa na Rais Xi” kama msingi wa kupatikana kwa amani na utulivu wa kikanda. Mapema mwaka huu, kiongozi huyo wa China alibainisha kanuni nne kwa ajili ya utulivu wa Asia Magharibi na Ghuba ya Uajemi, nazo ni: kuishi kwa amani, kuheshimu mamlaka ya kitaifa, kufuata sheria za kimataifa, na kusawazisha maendeleo na usalama, huku akithibitisha utayari wa China kuunga mkono mazungumzo na kuchukua nafasi yenye tija.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameema hali ya kikanda imepitia mabadiliko makubwa kufuatia vita haramu na vya kichokozi vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran mapema mwaka huu, akisema kuwa utaratibu mpya wa kikanda unapaswa kujengwa juu ya msingi wa ushirikiano miongoni mwa nchi za kikanda bila kuwepo kwa vikosi vya kijeshi vya kigeni au uingiliaji wa nje.

Amesisitiza: “Katika utaratibu mpya wa kikanda, ambao utaambatana na mazungumzo na ushirikiano miongoni mwa nchi za kikanda, hakuna nafasi kwa uwepo au uingiliaji wa vikosi vya kigeni.”

Katika mkutano huo wa Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi amesema kuwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran ni “haramu”. Aidha amesistiza umuhimu wa amani na utulivu katika eneo la Asia Magharibi na utatuzi wa masuala kupitia mazungumzo na diplomasia. Pia amesema China iko tayari kusaidia kupunguza mivutano na kuunga mkono mazungumzo.