Uganda yaanza kujenga kituo cha mafuta cha lita milioni 320
Jana Alkhamisi Uganda ilianza ujenzi wa kituo cha mafuta chenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 320. Kituo hicho kinajengwa katika wilaya ya Mpigi ya katikati mwa Uganda. Lengo la serikali ya Kampala ni kuimarisha usalama wa mafuta na usambazaji wake katika masoko ya ndani na ya ukanda mzima.
Hayo yametangaza na shirika la serikali la usambazaji mafuta nchini Uganda na kuongeza kuwa, Rais Yoweri Museveni ndiye aliyeongoza hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Kuhifadhi Mafuta cha Kampala (Kampala Storage Terminal) kitakachogharimu zaidi ya dola milioni 300. Kituo hicho kinajengwa na Shirika la Taifa la Mafuta la Uganda (UNOC).
Taarifa ya Ikulu ya Uganda imesema kuwa, Kituo hicho kitaongeza maradufu uwezo wa hivi sasa wa Uganda wa kuhifadhi mafuta, unaokadiriwa kuwa lita milioni 160. Rais Museveni amesema katika uzinduzi ya ujenzi wa kituo hicho kwamba, miundombinu ya kutosha ya kuhifadhi mafuta ni muhimu sana wakati huu ambapo Uganda inaendeleza sekta yake ya mafuta na kufanya kazi ya kuboresha usalama na ufanisi wa usambazaji wa mafuta. Amesema: "Kwa kuwa sasa tunapiga hatua nzuri katika kuendeleza rasilimali zetu, ni lazima tupange mipango ya kuhifadhi."
Naye Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Monica Musenero, amesema kuwa, kituo hicho kitatumika kama kitovu cha kimkakati cha kuhifadhi mafuta na kuimarisha mnyororo wa usambazaji wa mafuta nchini Uganda.
"Tunakaribisha ahadi ya UNOC ya kukamilisha mradi huu ndani ya miezi 24, na wizara yetu itaunga mkono ufanikishaji wa mradi huu," alisema Musenero.
Vilevile ametoa mwito wa kuboreshwa miundombinu ya barabara inayoelekea kwenye kituo hicho, hasa Barabara Kuu ya Mpigi pamoja na ujenzi wa miundombinu ya reli ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa za mafuta.