Ismail Haniya: Kambi za wakimbizi wa Kipalestina ni ngome za muqawama
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i63258-ismail_haniya_kambi_za_wakimbizi_wa_kipalestina_ni_ngome_za_muqawama
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, kambi za wakimbizi wa Kipalestina ni ngome za muqawama na kwamba, mpango wa kibaguzi wa Muamala wa Karne katu hautafanikiwa kufikia malengo yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 06, 2020 06:54 UTC
  • Ismail Haniya: Kambi za wakimbizi wa Kipalestina ni ngome za muqawama

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, kambi za wakimbizi wa Kipalestina ni ngome za muqawama na kwamba, mpango wa kibaguzi wa Muamala wa Karne katu hautafanikiwa kufikia malengo yake.

Ismail Haniya amesema hayo leo alipoitembelea kambi kubwa ya wakimbizi wa Kipalestina ya Ain al-Hilweh huko Lebanon na kueleza kwamba: Hatutasahau dhulma ya kihistoria na katu hatutasamehe kama ambavyo hatutasahau na kufumbia macho haki ya kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi za mabavu zao huko Palestina.

Haniya ameeleza kuwa, kambi za wakimbizi wa Kipalestina ni nembo na ngome za muqawama ambazo ndani yake hutokea matukio makubwa ya kihistroria, hulelewa na kuondokea mashujaa humo kama ambavyo katika kambi hizo kadhia ya Palestina huendelea kuwa hai.

Kiongozi huyo wa Hamas amemuonya adui Mzayuni na kueleza kuwa, muqawama katika Ukanda wa Gaza una makombora yanayoweza kupiga hadi Tel-Aviv na zaidi ya hapo.

Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS  akiwapungua mkono watu katika kambi ya wakimbizi ya Ain al-Hilweh Lebanon

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema pia kuwa, garimoshi la kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel lililoanza safari yake, siyo msimamo wa wananchi wote wa eneo kwani kadhia ya Palestina ingali katika nyoyo za wananchi wenye dhamira safi.

Wiki iliyopita kiongozi huyo wa HAMAS aliwasili katika mji mkuu wa Lebanon Beirut baada ya kupita miaka 27 ambapo mbali na kushiriki katika mkutano muhimu wa makundi ya muqawama, amekutana na kufanya mazungumzo pia na viongozi mbalimbali akiwemo Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon.