Qatar nayo yakataa kuchukua uwenyekiti wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
Serikali ya Qatar imekataa kuchukua uwenyekiti wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Arab League badala ya Palestina ambayo nayo ilikataa uwenyekiti huo ikilalamikia hatua ya baadhi ya mataifa ya jumuiya hiyo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.
Taarifa iliyotolewa leo na serikali ya Qatar imeeleza kuwa, nchi hiyo haitachukua uwenyekiti wa kiduru wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu badala ya Palestina iliyokuwa zamu yake kuongoza jumuiya hiyo.
Hatua ya nchi ya pili katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Arab League ya kukataa kuchukua uwenyekiti wa kiduru wa jumuiya hiyo inatahminiwa na wachambuzi wa mambo kuwa pigo kubwa kwa jumuiya hiyo na ishara ya wazi ya kuweko upinzani mkali dhidi ya mkumbo wa baadhi ya mataifa ya Kiarabu wa kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israe.
Hivi karibuni serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilitangaza kusamehe haki yake ya kuchukua uwenyekiti wa Arab League itaendelea kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo na kueleza kuwa, itaendelea kuwa mwanachama na haitajitoa licha ya hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu za kutangaza uhusiano wao wa kawaida na utawala wa Kizayuni, kwani kama itajitoa kutazidi kuzuka pengo katika ulimwengu wa Kiarabu.
Hivi karibuni nchi mbili za Kiarabu za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) pamoja na Bahrain zilitangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni. Usaliti huo umezusha hasira kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu na wa Kiarabu. Pamoja na hayo, katika kikao chake cha baada ya matukio hayo, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilikataa kulaani usaliti huo wa Imarati na Bahrain.