Shambulio kubwa lililofanywa na Israel bila ya onyo lolote laua Wapalestina 81 Ghaza
(last modified 2024-10-20T06:45:48+00:00 )
Oct 20, 2024 06:45 UTC
  • Shambulio kubwa lililofanywa na Israel bila ya onyo lolote laua Wapalestina 81 Ghaza

Wapalestina wasiopungua 81 wameuawa shahidi katika shambulizi la kinyama lililofanywa na jeshi katili la utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye mji wa Beit Lahiya kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.

Idara ya Habari ya Serikali ya Palestina katika ukanda huo imesema, watu wengi wangali wamekwama chini ya vifusi na idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka.

Taarifa za shambulio hilo la jeshi la Kizayuni zinatolewa katika hali ambayo, Beit Lahiya pamoja na Jabalia na Beit Hanoon, ambayo ni miji mitatu ya ncha ya kaskazini ya Ukanda wa Ghaza imekuwa chini ya mzingiro wa kijeshi wa Israel tangu siku 16 zilizopita, huku utawala huo wa Kizayuni ukizuia chakula, maji na vifaa vya matibabu kuingizwa katika miji hiyo mbali, na kukata mawasiliano ya simu na intaneti.

Kaskazini mwa Ghaza imekuwa ikiandamwa pia na mashambulizi makubwa ya jeshi la utawala ghasibu wa Israel, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya moja kwa moja yanayolenga hospitali yakiua na kujeruhi wagonjwa.

Kwa mujibu wa taarifa za karibuni za mashirika matatu ya kutetea haki za binadamu ya Palestina, wakazi wa kaskazini mwa Ghaza wana hofu kwamba hawataweza kurejea majumbani kwao iwapo watafuata "amri za Israel za kuwahamisha watu kwa nguvu" kinyume cha sheria.

Mashirika hayo ya kutetea haki za binadamu yanasema, mipango ya utawala wa Kizayuni ya kuinyakua na kuiunganisha Ghaza na maeneo mengine unayoyakalia kwa mabavu na kupeleka huko walowezi wa Kizayuni inazidi kudhihirika kadiri siku zinavyopita.

Wapalestina wapatao 42,519 wameshauawa shahidi hadi sasa na 99,637 wamejeruhiwa tangu utawala wa Kizayuni wa Israel ulipoanzisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya Ghaza Oktoba 7, 2023.../

 

Tags