UN: Sheria za kimataifa zinaitaka Israel kukomesha uvamizi huko Ukanda wa Gaza
(last modified 2024-10-19T08:02:30+00:00 )
Oct 19, 2024 08:02 UTC
  • UN: Sheria za kimataifa zinaitaka Israel kukomesha uvamizi huko Ukanda wa Gaza

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, nchi zote na mashirika ya kimataifa yana wajibu wa kukomesha uwepo haramu wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).

Tangu tarehe 7 Oktoba 2023, utawala wa Kizayuni ulianzisha vita vyenye uharibifu mkubwa dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza, vita ambavyo vimesababisha, maafa, uharibifu na njaa kali na kupelekea maelfu ya Wapalestina ambao wengi wao ni wanawake na watoto  kuuawa shahidi  na kujeruhiwa.

Navi Pillay, Mkuu wa Tume ya Baraza la Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, jana  Ijumaa,  aliziomba nchi zote kutekeleza kikamilifu azimio la Baraza Kuu la umoja huo ambalo liliidhinishwa mnamo Septemba 13, mwaka huu, na kusisitiza: "Nchi zote zina wajibu wa kukomesha uvamizi haramu  na kujaribu kudhamini kikamilifu haki ya watu wa Palestina ya kujitawala kwa kuzingatia sheria za kimataifa.

Akiashiria hatua zisizo sahihi za utawala katili wa  Israel na ukiukaji wake wa sheria za kimataifa katika Ukanda wa Gaza, mkuu huyo wa Baraza la Haki za Binadamu ameongeza kuwa, nchi zote zina wajibu wa kutotambua rasmi madai ya utawala wa Israel kuhusu ardhi au mamlaka yake juu ya ardhi zinazozikalia kwa mabavu na kupinga hatua zake za kukiuka sheria za kimataifa.

Navi Pillay ametoa wito wa kusitishwa misaada ya kifedha, kijeshi na kisiasa au uungaji mkono wa baadhi ya nchi kwa Israel na kusisitiza kuwa uungaji mkono na usaidizi huo kwa utawala wa Kizayuni unasaidia kuendelea kukalia kwa mabavu Palestina.

Tarehe 17 Septemba, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio katika mkutano wake wa 10 wa dharura ambapo lilitaka kusitishwa kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na utawala ghasibu wa Israel ndani ya mwaka mmoja.

Kwa kuidhalilisha jamii ya kimataifa na kupuuza maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kusitisha mara moja vita na maagizo ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ)  kuhusu ulazima wa kuzuia mauaji ya kimbari na kuboresha hali ya binadamu huko Gaza, Tel Aviv ingali inaendeleza jinai zake za kinyama huko Gaza.

Tags