UN: Kuwahamisha kwa mabavu raia kaskazini mwa Gaza ni jinai ya kivita
(last modified 2024-10-19T03:05:18+00:00 )
Oct 19, 2024 03:05 UTC
  • UN: Kuwahamisha kwa mabavu raia kaskazini mwa Gaza ni jinai ya kivita

Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa kitendo chochote cha kuwahamisha kwa nguvu raia wengi huko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza ni jinai ya kivita.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Volker Turk amesema akiwa makao makuu ya umoja huo mjini New York kuwa, huku mashambulizi ya jeshi la Israel yakiendelea, kuna wasiwasi mkubwa kuhusu kuhamishwa kwa nguvu raia wa Kipalestina; mchakato ambao haukidhi vigezo muhimu vinavyohitajika kwa mujibu wa sheria za kimataifa za uhamishaji raia kwa kuzingatia dharura ya kijeshi. 

Kamishna wa Haki za Binadamu wa UN ameitaka Israel iruhusu mara moja kupelekwa misaada mikubwa ya kibinadamu inayohitajika katika maeno yote ya Gaza.  

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu anazuia misaada ya kibinadamu kutumwa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, na maafisa wa kijeshi wa utawala huo ghasibu wamependekeza kuwa Wapalestina waliosalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza watambuuliwa kuwa ni "wanajeshi" na kwamba wanapasa kuuawa na kunyimwa chakula. 

Masaibu ya Wapalestina wa kaskazini mwa Gaza 

Kama mkakati huo utatekelezwa, mamia ya maelfu ya Wapalestina ambao hawataki au wameshindwa kuondoka katika makazi yao huko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza watazingirwa na jeshi la Israel. 

Jumamosi iliyopita wanajeshi wa utawala wa Israel walitoa amri mpya ya kuwahamisha raia wa Kipalestina ambao bado wanaishi kaskazini mwa Gaza; hata hivyo wakazi wengi wa eneo hilo wanasema kuwa vita na milio ya risasi imewafanya washindwe kuondoka.

Tags