UN: Watu bilioni 1 wanaishi katika umaskini wa kupindukia
(last modified 2024-10-18T02:51:03+00:00 )
Oct 18, 2024 02:51 UTC
  • UN: Watu bilioni 1 wanaishi katika umaskini wa kupindukia

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, zaidi ya watu bilioni moja wanaishi katika umaskini mkubwa, na karibu nusu yao wapo katika nchi zinazokumbwa na migogoro.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyochapishwa jana Alkhamisi na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP): Nchi zilizosumbuliwa na vita zina viwango vya juu vya uchochole katika viashiria vyote vya "umaskini wa pande nyingi".

Vigezo vya UN vya umaskini wa kupindukia vinazingatia tofauti "kubwa zaidi" katika lishe, upatikanaji wa umeme na nishati, maji na usafi wa mazingira.

Utafiti katika nchi 112 kwa kuwajumuisha watu bilioni 6.3 umebaini kuwa, watu bilioni 1.1 wanakabiliwa na umaskini, na milioni 455 kati yao wanaishi "katika kivuli cha migogoro".

Umaskini na uchochole Nigeria

Aidha ripoti hiyo imeeleza kuwa, asilimia 83.2 ya watu maskini zaidi duniani wanaishi kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika na Asia Kusini.

India ni nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaosakamwa na umaskini uliokithiri; ambapo watu milioni 234 kati ya watu wake bilioni 1.4 wanaandamwa na umaskini. Inafuatiwa na Pakistan, Ethiopia, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Nchi hizo tano kwa pamoja zilichangia karibu nusu ya watu maskini bilioni 1.1 wanaosumbuliwa na umaskini duniani.

Tags