Waziri Mkuu wa Malaysia alaani vikali mauaji ya Sinwar, asema nchi yake inaomboleza
(last modified 2024-10-20T02:46:04+00:00 )
Oct 20, 2024 02:46 UTC
  • Waziri Mkuu wa Malaysia alaani vikali mauaji ya Sinwar, asema nchi yake inaomboleza

Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim amelaani vikali mauaji ya kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar yaliyofanywa na vikosi vya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika taarifa aliyoweka kwenye mtandao wa kijamii wa X jana Jumamosi, Anwar amesema Malaysia inaomboleza kwa kumpoteza "mpiganaji na mtetezi wa watu wa Palestina."

Waziri Mkuu wa Malaysia amesisitiza katika taarifa hiyo aliyotoa kwa lugha ya Kimalay kwamba: "Malaysia ililaani vikali mauaji hayo, na ilikuwa dhahiri kwamba jaribio la utawala wa Kizayuni la kuzima takwa la kutolewa taarifa hiyo lisingefanikiwa. Malaysia inasisitiza kuwa jamii ya kimataifa inapinga ushenzi wa Israel na mauaji yanayoendelea ya Wapalestina lazima yakomeshwe mara moja".

Shahidi Yahya Sinwar

Katika sehemu nyingine ya taarifa yake hiyo, Anwar amesema, jamii ya kimataifa imeshindwa kuhakikisha amani na haki zinapatikana huku hali ikizidi kuwa mbaya katika eneo la Asia Magharibi; na kwamba licha ya sauti zinazopazwa kimataifa, Israel inaendelea na mashambulizi yake ya anga na ardhini huko Lebanon na Ghaza.

Wakati huo huo, serikali ya muda wa Taliban nchini Afghanistan nayo pia imetangaza kusikitishwa na kuuawa shahidi Yahay Sinwar, na kuutaka Ulimwengu wa Kiislamu usimame kimshikamano na watu wanaodhulumiwa wa Palestina.

"Tunatoa salamu zetu za rambirambi kwa Harakati ya Kiislamu ya Hamas, kwa mujahidina wote, na hasa kwa wapiganaji madhubuti wa Kipalestina, kwa kuuawa shahidi ndugu yetu mujahid shujaa, Yahya Sinwar," imeeleza taarifa ya Taliban.

Taarifa hiyo imeendelea kueleza: "tunatoa wito kwa Waislamu duniani kote kusimama kimshikamano na watu wanaodhulumiwa wa Palestina, kuunga mkono harakati zao, na kutimiza wajibu wa kidini ulioko juu yetu sote katika suala hili."

Siku ya Alkhamisi, jeshi la kigaidi la utawala haramu wa Israel lilimuua shahidi Yahya Sinwar katika mapigano makali yaliyojiri kati ya pande mbili huko Ghaza. Harakati ya Hamas ilithibitisha siku ya Ijumaa kifo cha kiongozi wake huyo kilichotokea kwenye mstari wa mbele wa vita, ikimtaja kuwa ni "shujaa ambaye alipigana na vikosi vya Israel hadi pumzi yake ya mwisho.../

Tags