Katika Siku ya Afya ya Akili Duniani, Katibu Mkuu wa UN asema: Hakuna afya bora bila afya ya akili
(last modified 2024-10-11T07:31:17+00:00 )
Oct 11, 2024 07:31 UTC
  • Katika Siku ya Afya ya Akili Duniani, Katibu Mkuu wa UN asema: Hakuna afya bora bila afya ya akili

Siku ya Afya ya Akili Duniani imeadhimishwa Oktoba 10 huku ikiripotiwa kuwa, mtu mmoja kati ya wanane duniani ana tatizo la afya ya akili.

Katika ujumbe aliotoa kwa mnasaba wa siku hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, kwa kuzingatia takwimu hizo, hakuna jamii au eneo ambalo liko salama huku akitanabahisha kuwa, kujiua ingali ndiyo sababu kuu ya vifo miongoni mwa vijana na mamilioni wanaendelea kutatizwa na afya ya akili kimya kimya.

Kwa kuzingatia hali hiyo Guterres amesema, Siku ya Afya ya Akili Duniani mwaka huu inajikita katika afya ya akili pahala pa kazi.

“Asilimia 60 ya watu walio na umri wa zaidi ya miaka 15 wanatumia muda wao mwingi wakiwa pahala pa kazi. Maeneo haya ni mahala ambapo ni zaidi ya pahala pa kazi,” amesisitiza Katibu Mkuu huyo wa UN. 

Antonio Guterres

Guterres ameongeza kuwa,  mahala pa kazi palipo salama na penye afya panaweza kumpatia mfu fursa ya kutambua lengo lake, kupata mtandao na utulivu; ilhali mazingira ya kazi kandamizi au yenye vurugu yanaweza kuwa na madhara makubwa kwenye afya ya akili kwa wafanyakazi walioko eneo hilo.

Aidha, amekumbusha kuwa, hakuna afya bora bila afya ya akili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, uwekezaji kwenye afya ya akili ungali ni mdogo na watu wengi bado wanakabiliwa na unyanyapaa na kubaguliwa.

Aidha, ametaja mazingira yasiyo rafiki pahala pa kazi pamoja na uonevu, unyanyasaji na ubaguzi wa rangi na mashinikizo akisema, vinaweza kudhuru afya ya akili.../

 

 

 

Tags