Ujumbe wa kuhuishwa uhusiano wa kidiplomasia wa Oman na Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i63843-ujumbe_wa_kuhuishwa_uhusiano_wa_kidiplomasia_wa_oman_na_syria
Turki bin Mahmood al-Busaidy ambaye ameteuliwa kuwa balozi maalumu wa Oman nchini Syria siku ya Jumapili Oktoba 4 alikabidhi nyaraka zake za ubalozi kwa Walid Al Muallim, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 05, 2020 21:27 UTC
  • Ujumbe wa kuhuishwa uhusiano wa kidiplomasia wa Oman na Syria

Turki bin Mahmood al-Busaidy ambaye ameteuliwa kuwa balozi maalumu wa Oman nchini Syria siku ya Jumapili Oktoba 4 alikabidhi nyaraka zake za ubalozi kwa Walid Al Muallim, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria.

Hatua ya Oman ya kurejesha balozi wake huko Syria ina jumbe kadhaa muhimu.

Kuarifishwa balozi mpya wa Oman nchini Syria ni miongoni mwa hatua za kwanza zilizochukuliwa na Haitham bin Tariq as-Said, Mfalme wa Oman, baada ya kuingia madarakani mwezi Januari mwaka huu kufuatia kifo cha mfalme wa zamani wa nchi hiyo Sultan Qabus. Hatua hiyo bila shaka inathibitisha wazi kwamba katika kipindi hiki kipya cha uongozi, Oman inataka kuwa na uhusiano mzuri na nchi zote za Mashariki ya Kati, ikiwemo Syria. Kuhusu suala hilo Turki bin Mahmood al-Busaidy katika mazungumzo yake na Walid Muallim, amebadilishana mawazo na waziri huyo kuhusu njia za kuimarisha ushirikiano wa nchi mbili katika nyanja tofauti.

Nukta nyingine ni kwamba hatua ya Oman kumuarifisha balozi wake mpya nchini Syria inathibitisha wazi kushindwa mashinikizo ya nchi za Kiarabu ya kutaka kuitenga serikali ya Damascus. Saudi Arabia na nchi nyingine kadhaa za Kiarabu zilikuwa na nafasi muhimu katika matukio ya 2011 ambayo yaliibua vita vya makundi ya kigaidi dhidi ya serikali hiyo. Mbali na kuyaunga mkono kwa hali na mali makundi hayo, Saudia ilikuwa na nafasi muhimu katika kuongeza mashinikizo ya kisiasa dhidi ya serikali ya Damascus ambapo pamoja na mambo mengine, ilichochea kuondolewa kwake katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Arab League, na wakati huohuo kuzishinikiza nchi za Kiarabu ziondoe mabalozi wao nchini Syria. Uanachama wa nchi hiyo ulisimamishwa katika jumuiya hiyo licha ya kuwa ni moja ya nchi zilizoiasisi mnamo mwaka 1945.

Turki bin Mahmood al-Busaidy akimkabidhi Walid Muallim nyaraka zake za utambulisho

Baada ya kupita miaka 7 ya mgogoro wa Syria na serikali ya Rais Bashar a-Asad kupata uthabiti mkubwa wa kisiasa, mwaka 2018 nchi za Imarati na Bahrain ambazo katika muongo mmoja uliopita zimekuwa zikifuata siasa za uhasama za Saudi Arabia dhidi ya Syria, ziliamua kufungua balozi zao mjini Damascus. Pampja na hayo nchi mbili hizo bado hazijawarejesha mabalozi wao mjini humo na suala la Syria kurejeshewa uanachama wake katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pia bado halijulikani vizuri. Kuhusu maudhui hiyo, Ahmad Abulghait, Katibu Mkuu wa Arab League alisema hivi karibuni kwamba uamuazi kuhusiana na jambo hilo bado haujachukuliwa.

Tukiachilia mbali suala la iwapo Syria itarejeshewa uanachama wake katika jumuiya hiyo au iwapo nchi za Imarati na Bahrain zitawaarifisha mabalozi wao wapya mjini Damascus au la, hatua ya Oman ya kumtangaza balozi wake mpya mjini humo ni ishara ya wazi ya kushindwa mashinikizo ya kistratijia ya nchi za Kiarabu dhidi ya Syria au kwa uchache ni dalili ya kuongezeka hitilafu kati ya nchi hizo kuhusu kadhia ya kuhuishwa uhusiano wa kidiplomasia na Damascus. Mbali na hayo hatua hiyo ya Oman pia inathibitisha kwamba serikali ya Syria imefanikiwa pakubwa kupata uthabiti wa kisiasa na hivyo kuweka pembeni hatari ya kubadilishwa mfumo wa utawala wa nchi hiyo. wakati huo huo hatua hiyo ya Oman inaashiria kushindwa kwa siasa za uhasama na za kuzua migogoro za Saudia nchini Syria kama zilivyoshindwa pia nchini Yemen.

Baadhi ya nchi za Kiarabu zimetia saini mikataba ya kusaliti maslahi ya ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu

Nukta ya mwisho ni kwamba siasa za hujuma na kijeshi ambazo zimekuwa zikitekelezwa dhidi ya Syria kwa muongo mmoja uliopita, hazijakuwa na natija nyingine ghairi ya kuudhoofisha utambulisho wa ulimwengu wa Kiarabu, kuhatarisha maslahi na usalama wake pamoja na kupanua pengo la hitilafu la nchi za Kiarabu. Suala hilo limeunufaisha tu utawala haramu wa Israel kwa kadiri kwamba nchi za Kiarabu zimegawanyika na kushindwa kuchukua hatua  yoyote ya kupinga uamuzi wa Marekani wa kutwaa ardhi za Warabu na kuukabidhi utawala ghasibu wa Israel kupitia mpango wa aibu na fedheha wa eti Muamala wa Karne. Jambo la kushangaza na kuaibisha zaidi ni kuwa nchi hizo zimedhalilishwa zaidi kwa kulazimishwa kukubali kuboresha uhusiano wao wa kidiplomasia na utawala huo wa Kizayuni. Kabla ya jambo lolote lile, hali hii ya kusikitisha imesababishwa na siasa mbovu za nchi za Kiarabu na hasa Saudi Arabia kuhusiana na mgogoro wa Syria.