Mwanamfalme wa Saudia akerwa na Palestina kupinga uhusiano na Israel
Mkuu wa zamani wa Idara ya Ujasusi ya Saudi Arabia amewakosoa vikali viongozi wa Palestina kwa kupinga hatua ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.
Katika mahojiano na Televisheni ya al-Arabiya ya Saudia, Mwanamfalme Bandar bin Sultan bin Abdulaziz ambaye ni afisa wa ngazi ya juu wa utawala kiuukoo wa Aal-Saud amesema, kitendo hicho cha viongozi wa Palestina kupinga kuanzishwa uhusiano na Tel Aviv kinaenda kinyume na kanuni na kinapaswa kulaaniwa.
Mwanamfalme huyo ambaye amewahi pia kuwa Balozi wa Saudia nchini Marekani amedai kuwa, "hatukutaraji haya kutoka kwa maafisa (wa Palestina) ambao wanataka kadhia yao ipate uungaji mkono wa kimataifa."
Bandar bin Sultan bin Abdulaziz ametoa matamshi ya kukinzana kwa kusema: Kadhia ya Palestina ni kadhia ya haki, lakini wanaoipigania ni watu waliofeli; na kadhia ya Israel si ya haki lakini watetezi wake wameonekana kufaulu. Huo ndio mukhtasarari wa matukio yaliyofanyika katika kipindi cha miaka 70 hadi 75 iliyopita.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa utawala wa Riyadh ametoa kauli hiyo katika hali ambayo, ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu unaendelea kulaani hatua ya Imarati na Bahrain kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni.
Waislamu na wapenda haki kote duniani wamekitaja kitendo hicho cha UAE na Bahrain kama usaliti na ni sawa na kuwachoma jambia kwa nyuma wananchi madhulumu wa Palestina.