EU yaishurutisha Palestina kulipa kodi kwa Israel ili iendelee kuisaidia kifedha
Umoja wa Ulaya umesema utaipatia Palestina msaada wa fedha kwa sharti la kulipa kodi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameieleza Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuwa, misaada zaidi ya kifedha ya umoja huo itatolewa kwa sharti la mamlaka hiyo kuanzisha uhusiano wa kiuchumi na Israel na kulipa kodi kwa Tel Aviv.
Kwa mujibu wa tangazo la Umoja wa Ulaya, kutokana na kuondolewa mpango wa kupora eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan kwenye ajenda ya utekelezaji ya utawala wa Kizayuni, Mamlaka ya Ndani ya Palestina inapaswa ikubali kuilipa wizara ya fedha ya Israel kodi ya dola milioni 750.
Hayo yanaripotiwa wakati Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alitangaza mwezi Mei mwaka huu kwamba, kufutaia uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kumega asilimia 30 ya ardhi ya Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, mamlaka hiyo inabatilisha makubaliano iliyofikia na utawala huo haramu na Marekani na kuvunja mashirikiano ya kiusalama na kiraia iliyofikia na pande mbili hizo.
Kufuatia uamuzi huo wa utawala wa Kizayuni, Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeamua kusitisha ukusanyaji kodi wa kila mwezi wa dola milioni 150 kwa wananchi wa Wapalestina ambazo ilikuwa ikiulipa utawala haramu wa Israel.
Mbali na kupinga sharti hilo la Umoja wa Ulaya, Mahmoud Abbas amesisitiza kuwa, hatotekeleza sharti jengine lolote lile kabla Israel kutoa hakikisho kwa maandishi la kubatilisha mpango wa kumega asilimia 30 ya ardhi ya Ufukwe wa Magharibi na kuiunganisha na ardhi zingine za Palestina inazozikalia kwa mabavu.
Katika wiki za karibuni, Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeuomba Umoja wa Ulaya na nchi kadhaa za Ulaya ziipatie mikopo ya fedha kwa ajili ya kulipa mishahara ya wafanyakazi wake.../