Oct 09, 2020 02:36 UTC
  • Taathira hasi za kuendelea vita eneo la kusini mwa Kavkazia

Kwa kuendelea mapigano baina ya Jamhuri ya Azeribaijan na Armenia, hivi sasa pande hasimu katika vita zimepanua wigo kutoka ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kuingia katika maeneo yenye umuhimu wa kiuchumi.

Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuongezeka raia waliouawa katika mapigano huku maeneo ya kiuchumi yakipata hasara. Katika hali kama hiyo serikali za kieneo hasa Iran na Russia zimetoa wito kwa pande zinazopigana kuketi kwenye meza ya mazungumzo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewasilisha mpango wenye lengo la kuhitimisha mapigano baina ya nchi hizo mbili zinazopakana na Iran. Wakuu wa  Wizara ya ya Mambo ya Nje ya Iran wameimarisha maradufu jitihada za kuzishawishi pande mbili hasimu ziafiki mpango wa amani wa Iran.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeimarisha maradufu jitihada za kuwasilisha mpango wa amani kwa pande zinazohasimiana huko Nagorno-Karabakh kwa sababu baadhi ya duru rasmi za habari zimedokeza kuwa wanamgambo wanaofungamana na magaidi walioko Syria na Iraq wamefika katika eneo la kusini mwa Kavkazia. Kuhusiana na nukta hii, Mkuu wa Idara ya Russia ya Ujasusi wa Nje ya Nchi amebainisha wasi wasi kuhusu kugeuka eneo la Nagorno-Karabakh kuwa njia ya magaidi kujipenyeza katika nchi jirani. 

Sergei Naryshkin, Mkuu wa Idara ya Russia ya Ujasusi wa Nje ya Nchi amesema: "Kuenea wigo wa mapigano katika eneo la Nagorno-Karabakh ni kama sumaku kwani mapigano hayo yanawavutia wanamgambo kutoka makundi mbali mbali ya kigaidi na kimataifa ambao wanafika katika eneo hilo kwa matumaini ya kupata malipo kupigana. Wanamgambo hao wanaweza kutumia Jamhuri ya Azerbaijan na Armenia kuingia katika nchi jirani ikiwemo Russia na jambo hilo linaibua wasi wasi mkubwa."

Katika kipindi cha siku chache zilizopita, duru za habari  na za maafisa wa serikali za eneo zimedokeza kuwa, utawala haramu wa Israel unatekeleza jitihada maalumu za kuwatuma magaidi katika eneo la Kavkazia. Wakuu wa Russia wamebainisha wasi wasi wao katika hali ambayo Uturuki ni nchi pekee ya eneo inayomshawishi wazi wazi Rais Ilham Aliyev wa Jamhuri ya Azerbaijan aendeleza mapigano. Hivyo ni wazi kuwa hatua hii ya serikali ya Uturuki inatekelezwa ili kuiwezesha kueneza satwa yake katika eneo la Kavkazia Kusini kupitia mapigano baina ya Jamhuri ya Azerbaijan na Armenia. Haya ni mapigano ambayo yanaweza kumalizika kwa hasara kubwa ya kibinadamu na kifedha baina ya pande mbili hasimu. Kwa hivyo kuichochea Jamhuri ya Azerbaijan iendeleze mapigano na kutozingatia mipango ya amani ni jambo ambalo litaisababishia hasara kubwa nchi hii ya Waislamu.

Iran imewasilisha mpango wa amani kwa pande mbili hasimu katika hali ambayo viongozi wa Jamhuri ya Azerbaijan na Armenia kwa miaka kadhaa sasa wamekuwa wakikosoa upuuzaji wa 'Kundi la Minsk' katika Shirika la Usalama na Ushirikiano Barani Ulaya (OSCE) kuhusu utatuzi wa mgororo wa muda mrefu wa Nagorno-Karabakh. Pamoja na hayo, inaelekea kuwa viongozi wa 'Kundi la Minsk' yaani Russia, France, na Marekani wanaunga mkono msimamo wa Armenia wa kufanyika mazungumzo ya amani kuhusu mgogoro wa Nagorno-Karabakh. Uungaji mkono huu umepelekea wakuu wa Jamhuri ya Azerbaijan kutokuwa na imani na 'Kundi la Minsk'. Hapa tunaweza kuashiria mitazamo ya weledi wa mambo ambao wako karibu na serikali ya Ilham Aliyev. Kwa mfano Avziri Jafarov mtaalamu wa masuala ya kijeshi katika Jamhuri ya Azerbaijan anasema: "Kwa kuzingatia upendeleaji unaoonyeshwa na viongozi wa 'Kundi la Minsk' hakuna matumaini kuhusu utatuzi wa tatizo la Nagorno-Karabakh.

Bendera za nchi wanachama wa Shirika la Usalama na Ushirikiano Barani Ulaya (OSCE

Mtaalamu huyu wa masuala ya kijeshi amesema nchi za Magharibi zinatetea maslahi ya serikali ya Armenia na Waarmenia wanaoishi katika eneo la Nagorno-Karabakh. Anaongeza kuwa:  Baada ya kupita zaidi ya miongo miwili, watu wa Jamhuri ya Azerbaijan na wakuu wa nchi hiyo hawana imani tena na upatanishi wa 'Kundi la Minsk.'

Kwa ujumla, muelekeo wa mapigano ya sasa na utendaji wa serikali za eneo na dunia unaonyesha kupoteza matumaini pande hasimu katika mgogoro wa Nagorno-Karabakh. Huku madola ajinabi yakiendelea kuzichochea pande mbili hasimu ziendelee na vita kuna wasi wasi kuwa, kutakuwa na vizingiti daima vya kufikiwa amani baina ya pande mbili.

Tags