Palestina katika njia ya umoja na mshikamano wa ndani
Baada ya baadhi ya nchi za Kiarabu kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na kulitelekeza waziwazi taifa la Palestina, sasa hivi makundi ya Palestina yameelewa kuwa njia pekee ya kulinda uwepo wa taifa lao ni umoja na mshikamano.
Katika miaka ya hivi karibuni, nchi za Kiarabu zimeimarisha mno uhusiano wao wa siri na utawala wa Kizayuni lakini zimeona hayo yote hayatoshi, hivyo zimeamua kutangaza hadharani uhusiano wao huo. Gazeti la Kizayuni la Maariv limeandika: "Uhusiano rasmi wa siri baina ya utawala wa Kizayuni na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) umekuwepo kwa zaidi yamiaka 20, ni sasa hivi tu ndipo umetangazwa waziwazi."
Pamoja na hayo, tukio lililotokea hivi karibuni yaani tarehe 15 Septemba 2020 la kutiwa saini rasmi uhusiano wa kawaida baina ya nchi mbili za Kiarabu za Imarati na Bahrain na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ikulu ya Marekani, White House, limewapa mshituko mkubwa Wapalestina. Si kwamba Wapalestina hawakuwa wanatarajia jambo hilo, la, lakini sasa wameelewa kwamba nchi za Kiarabu hazilipi umuhimu wowote suala la kulindwa muundo wa kijiografia wa ardhi ya Palestina.
Kwa kweli sasa Wapalestina wameelewa kwamba njia pekee ya kulinda uwepo wao ni mshikamano na kusaidiana wao kwa wao. Wameelewa kuwa hiyo ndiyo sunna ya kimataifa ya kwamba kila nchi lazima ijitegemee kulinda uwepo wake, kwani kutegemea wengine hakuna matunda yoyote zaidi ya kujidhalilisha. Wameelewa kwamba uwepo wa taifa la Palestina hauwezi kutegemea misimamo ya nchi kama Imarati, Bahrain na nchi mithili ya hizo ambazo ni vibaraka wa madola ya kibeberu hasa Marekani ambayo ni maadui wakubwa wa taifa la Palestina. Baada ya makundi ya Palestina kuelewa uhakika huo, sasa tunayaona makundi hayo yakielekea zaidi upande wa mshikamano na umoja baina yao. Lugha inayotumiwa sana sasa hivi na makundi ya Palestina ni umoja wa kitaifa, utambulisho wa kisiasa na utambulisho wa kitaifa.
Awali viongozi na wakurugenzi wa makundi yote 14 ya Palestina, tarehe pili Septemba 2020 walifanya kikao cha kwanza kabisa cha kitaifa baada ya kupita zaidi ya miaka 20. Kikao hicho kilifanyika mjini Beirut Lebanon na makundi yote, kwa umoja wao, yalitilia mkazo wajibu wa kuwa na muqawama amilifu wa kukabiliana na njama za aina tatu za Muamala wa Karne, kupora ardhi zaidi za Wapalestina na kutangaza uhusiano wa kawaida.
Hatua iliyofuatia ilikuwa ni kikao baina ya viongozi wa harakati za HAMAS na Fat'h kilichofanyika mwishoni mwa mwezi Septemba nchini Uturuki. Kikao hicho kilikuwa muhimu sana hasa kutokana na harakati hizo mbili kila moja kuwa na ngome katika moja ya pande mbili kuu a Palestina yaani Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza. Mwishoni mwa kikao cha Uturuki, harakati hizo mbili za Palestina zilitangaza kuwa zimekubaliana kushirikiana ili kuhakikisha kunafanyika mazungumzo ya kitaifa yatakayoshirikisha mirengo yote ya Palestina. Fat'h na HAMAS zilitangaza pia kuwa, zimekubaliana kumaliza migawanyiko na hitilafu katika safu za Wapalestina, kuitisha uchaguzi na kuandaa mpango maalumu wa kitaifa wa kukabiliana na changamoto zinazolikumba taifa la Palestina.
Katika hatua ya tatu, makundi yote ya Palestina yameamua kuitisha kikao cha pamoja huko Moscow, mji mkuu wa Russia kwa mwaliko wa viongozi wa nchi hiyo.
Kwa kumailizia ni vyema kusema kwamba, ijapokuwa njama tatu kuu za Muamala wa Karne, kuteka ardhi zaidi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi na kutangaza uhusiano wa kawaida na Wazayuni ni tishio kwa uwepo wa taifa la Palestina, lakini inaonekana kwamba njama hizo zimesababisha kutokea mabadiliko ya kimsingi na kuangaliwa upya misimamo ya mirengo na mkundi ya Palestina. Sasa hivi misimamo ya makundi yote ya Palestina ni umoja na mshikamano wa kitaifa kwa ajili ya kulinda uwepo wa taifa lao na kutotarajia chochote chema kutoka kwa viongozi wa nchi za Kiarabu.