MSF: Israel inaendelea kutumia misaada ya Gaza kama silaha ya vita
Afisa mkuu wa shirika la kimataifa la misaada ya kibinadamu la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) anasema utawala wa Israel unaendelea kutumia misaada ya kibinadamu huko Gaza kama silaha ya vita dhidi ya Wapalestina.
Caroline Willemen alisistiza jana katika taarifa kwamba misaada inayotumwa katika Ukanda wa Gaza haipaswi kuhusishwa na hali yoyote ya kisiasa.
Bi Caroline Willemen ameeleza kuwa mashambulio ya Israel katika Ukanda wa Gaza yamepungua tangu kuidhinishwa ustishaji vita huko Gaza, lakini utawala huo tarehe 19 Oktoba ulifanya shambulizi kubwa, na kwamba karibu kila siku jeshi la Israel linatekeleza mashambulizi huko Gaza.
"Hali ya kibinadamu huko Gaza bado haijaboreka kwa kiasi kikuwa. Bado eneo hilo linasumbuliwa na uhaba wa maji, na majira ya baridi yanapokaribia, mamia ya maelfu ya watu bado wakiishi kwenye mahema", amesema Mratibu wa Miradi wa shirika la kkimataifa la misaada ya kIbinadamu la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF).
Bi Caroline Willemen amesisitiza kuwa timu za shirika la MSF zinaendelea kusajili idadi ya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito walioathiriwa na utapiamlo mkali. Amesema, hali ya lishe bado inatia wasiwasi katika Ukanda wa Gaza licha ya ongezeko dogo la upatikanaji wa chakula.