Iran yaalani shambulio la kigaidi Kabul, watu 18 wapoteza maisha
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64222-iran_yaalani_shambulio_la_kigaidi_kabul_watu_18_wapoteza_maisha
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana usiku alilaani shambulio la kigaidi lililotekelezwa huko Kabul mji mkuu wa Afghanistan na kutoa pole kwa serikali, wananchi na familia za wahanga wa jinai hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 25, 2020 04:19 UTC
  • Iran yaalani shambulio la kigaidi Kabul, watu 18 wapoteza maisha

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana usiku alilaani shambulio la kigaidi lililotekelezwa huko Kabul mji mkuu wa Afghanistan na kutoa pole kwa serikali, wananchi na familia za wahanga wa jinai hiyo.

Saeed Khatibzadeh ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Wanafunzi wa Kiafghani wamekuwa wahanga wa vitendo vya ukatili na vita visivyo na ukomo ambavyo kamwe hawakuvichagua. Amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vikali jinai hiyo ya kutisha na kutoa pole kwa wananchi na serikali ya Afghanistan.  

Khatibzadeh pia alisema: "Usiku huu Iran inaiomboleza Afghanistan." 

Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Afghanistan pia  umetoa taarifa na kulaani shambulio la kigaidi lilitekelezwa katika kituo cha elimu cha Kauthar magharibi mwa Kabul na kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga na kuwaombea afya njema na afueni majeruhi wa shambulio hilo la kigaidi.  

Shambulio la kigaidi katika kituo cha mafunzo cha Kauthar Danesh mjini Kabul 

Mtu mmoja aliyekuwa amejifunga bomu jana alasiri alijilipua karibu na kituo cha mafunzo cha Kauthar- Danesh katika eneo la Dasht-e-Barchi magharibi mwa mji mkuu, Kabul. Watu wasiopungua 18 wameuawa na 57 kujeruhiwa katika shambulio hilo lal kigaidi. Aghalabu ya wahanga wa mlipuko huo wa kigaidi walikuwa vijana waliokuwa wakipata mafunzo kituoni hapo.