Harakati za Palestina zalaani mateka Mpalestina kufia gerezani
Makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina yametoa taarifa na kulaani kufa shahidi mateka Mpalestina Kamal Abu Waar akiwa katika jela ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema hilo ni thibitisho la namna utawala huo unavyowatendea unyama wafungwa.
Jumuiya ya 'Sauti ya Mateka" ilitangaza Jumanne kuwa, Kamal Abu Waar mateka Mpalestina ambaye kwa muda mrefu sana amekuwa akiugua saratani amefariki dunia baada ya kuambukizwa corona na kufuatia uzembe wa kitiba katika gereza la Israel la Jalbout.
Kwa mujibu wa Kituo cha Upashaji Habari cha Palestina, Hazem Qassem Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, siku ya Jumanne usiku alitoa taarifa na kusema kufa shahidi Kamal Abu Waar kumepelekea idadi ya wafungwa waliokufa shahidi kufika 226 na hii ni dalili ya wazi kuwa jinai za kivita za utawala wa Kizayuni dhidi ya wafungwa Wapalestina zingali zinaendelea.
Kamati ya Mapambano ya Palestina nayo imetoa taarifa na kusema kufa shahidi Abu Waar ni matokeo ya sera za uzembe wa kitiba na ubaguzi wa wazi wa adui Mzayuni. Kamati hiyo imesema magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel yamekuwa yakikiuka sheria za kimataifa kwa makusudi kwa kuwakandamiza na kuwanyima haki mateka Wapalestina.
Nayo Harakati ya Uhuru wa Palestina imesema kufa shahidi Abu Waar ni jinai nyingine ya Israel katika orodha ndefu ya jinai zake.
Karibu mateka 4,800 wa Palestina wakiwemo wanawake 41 na watoto 140 wanashikiliwa katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel. Mateka hao wa Palestina ni kati ya waathirika wakubwa wa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Inakadiriwa kuwa tokea mwaka 1967, Wapalestina 226 wamekufa shahidi katika jela za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Tokea zamani mateka Wapalestina wamekuwa wakiishi katika hali mbaya sana katika magereza ya utawala wa Israel na sasa baada ya kuibuka janga la corona hali yao imezidi kuwa mbaya.
Utawala wa Israel umekataa kuwapa mateka Wapalestina huduma na suhula za afya. Moja ya hatua zilizo dhidi ya binadamu ambazo Israel imezichukua dhidi ya mateka Wapalestina ni kuwatuma madaktari walioambukizwa corona kuhudumu katika magereza hayo.