Wasiwasi wa Baraza la Usalama kuhusu kuongezeka mgogoro wa Yemen
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limebainisha wasiwasi wake kuhusu kushadidi mivutano ya kijeshi na uhaba wa chakula nchini Yemen.
Baraza hilo limetoa taarifa na bila ya kuashiria jinai za kutisha zinazofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen limesema: Wanachama wa baraza hili wanalaani mivutano ya kijeshi inayoendelea Yemen.
Wanachama hao wamedai katika taarifa hiyo kwamba jamii ya kimataifa inasisitiza na kuunga mkono kikamilifu haki ya kujitawala, umoja, uhuru na ardhi yote ya Yemen.
Taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imesema kwamba watu wapatao milioni 13.5 wa Yemen wanakabiliwa na hatari kubwa ya janga la njaa kutokana na uhaba mkubwa wa chakula uliopo katika nchi hiyo masikini ya Kiarabu.
Imesema kwamba huenda idadi hiyo ikaongezeka na kufikia watu milioni 16 ifikapo Juni 2021.
Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vile vile wameeleza wasi wasi walionao kuhusiana na ripoti zinazosema kwamba huenda Yemen ikabiliwa na hata janga kubwa zaidi la baa la njaa kutokana na kupungua kwa bajeti ya kununulia chakula kwa ajili ya watu wa nchi hiyo. Wamezitaka nchi zote fadhili zitekeleze ahadi zao za kuwasaidia Wayemen.
Saudi Arabia kwa uungaji mkono wa Marekani na nchi nyingine kadhaa, iliishambulia Yemen mwezi Machi 2015 na kuizingira katika pande zote za nchi kavu, anga na bahari, na kupelekea Wayemen zaidi ya elfu 16 kuuawa, makumi ya maelfu kujeruhiwa na mamilioni ya wengine kulazimishwa kuwa wakimbizi.