Uturuki yamteua balozi mpya wa Israel baada ya miaka 2
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i65192-uturuki_yamteua_balozi_mpya_wa_israel_baada_ya_miaka_2
Uturuki imemteua balozi wake mpya wa Tel Aviv, zaidi ya miaka miwili baada ya Ankara kumuita nyumbani balozi wake aliyekuweko katika utawala haramu wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 14, 2020 08:48 UTC
  • Uturuki yamteua balozi mpya wa Israel baada ya miaka 2

Uturuki imemteua balozi wake mpya wa Tel Aviv, zaidi ya miaka miwili baada ya Ankara kumuita nyumbani balozi wake aliyekuweko katika utawala haramu wa Israel.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Al-Monitor, Uturuki imemteua balozi mpya anayetazamiwa kujaza nafasi iliyoachwa wazi mwaka 2018, baada ya Ankara kumrejesha nyumbani balozi wake aliyekuweko Tel Aviv, kwa madai ya kuuawa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na pia kulalamikia hatua ya Marekani ya kuuhamishia ubalozi wake Quds Tukufu kutoka Tel Aviv.

Duru za habari zinaarifu kuwa, licha ya Uturuki na Israel kukwaruzana na kuwarejesha nyumbani mabalozi wao zaidi ya miaka miwili iliyopita, lakini hivi sasa pande mbili hizo zimeanza tena kuhuisha uhusiano wao.

Habari zaidi zinaarifu kuwa, anayetazamiwa kuwa balozi mpya wa Uturuki mjini Tel Aviv ni mwanakademia, Ufuk Ulutas, Mwenyekiti wa Kituo cha Utafiti wa Kistratejia cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki.

Maandamano dhidi ya Israel nchini Uturuki

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, lengo la Uturuki la kutaka kuhuisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Israel ni kutaka kujikurubisha kwa Marekani na Umoja wa Ulaya, ikidhani kuwa hilo litaifanya iondokane na mgogoro wa kiuchumi unaoikabili.

Hii ni katika hali ambayo, Morocco ndiyo nchi ya hivi karibuni kabisa ya Kiarabu kufuata mkumbo wa Sudan, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu wa kuanzisha uhusiano na utawala huo wa Kizayuni.