Saudia yamrejesha kazini kimya kimya muuaji wa Jamal Khashoggi
Mshukiwa mkuu wa mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari raia wa Saudia aliyeuliwa kinyama ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki mwaka 2018 amerejeshwa kazini kimya kimya.
Tovuti inayofichua habari za ndani ya utawala wa kiukoo wa Aal-Saud ya Al-Ahd Al-Jadeed imeandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa: Saud bin Abdullah al-Qahtani, mmoja wa washukiwa wakuu wa mauaji ya Khashoggi amerejeshwa katika wadhifa wake wa kusimamia vyombo vya mahakama nchini Saudia.
Al-Qahtani amerejeshwa kazini kimya kimya, miaka miwili baada ya kutoonekana hadharani na katika vyombo vya habari, na pia miezi kadhaa baada ya kutolewa hukumu ya kimaonyesho dhidi yake na watuhumiwa wengine wa mauaji ya Khashoggi.
Machi mwaka huu, Mahakama ya Uturuki ilianza kusikiliza kesi ya maafisa 20 wa Saudi Arabia walioshtakiwa kwa mauaji ya Jamal Khashoggi, akiwemo al-Qahtani ambaye pia ni mshauri wa zamani wa mahakama ya kifalme na masuala ya vyombo vya habari wa Saudia ambaye alishtakiwa kwa kuchochea na kuongoza operesheni kwa kutoa amri na maagizo kwa kikosi cha mauaji ya Khashoggi.
Waendesha Mashtaka wa Uturuki wameshatoa waranti wa kukamatwa washtakiwa hao wa mauji ya kinyama ya Khashoggi, akiwemo al-Qahtani.
Mkosoaji huyo wa Mrithi wa Ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman aliuawa kwa njia ya kutisha mnamo tarehe 2 Oktoba mwaka 2018 akiwa ndani ya jengo la ubalozi wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki na mwili wake ukakatwa vipande vipande.