Bin Salman na Bin Zayed wafanya kikao cha faragha kuijadili Qatar
(last modified Sun, 20 Dec 2020 13:58:17 GMT )
Dec 20, 2020 13:58 UTC
  • Bin Salman na Bin Zayed wafanya kikao cha faragha kuijadili Qatar

Baadhi ya duru za kuaminika zimeripoti kuwa mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia na mwenzake wa Imarati (UAE) wamefanya kikao cha faragha cha kuzungumzia kadhia ya Qatar.

Kwa mujibu wa Al-Khaleej Al-Jadid, duru za kuaminika zimetangaza kuwa, Mohammad bin Zayed, mrithi wa ufalme wa Imarati na Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia wamekutana kwa mazungumzo katika mji wa Neom ulioko kwenye pwani ya Bahari Nyekundu na tayari wamefikia makubaliano yasiyo rasmi kuhusu kadhia ya Qatar.

Kabla ya hapo, vyombo vya habari vilikuwa vimeripoti kuwa, kikao cha kila mwaka cha wakuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi GCC kimeakhirishwa hadi mwezi Januari 2021 kwa sababu ya uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya msingi kwa ajili ya kutatua mgogoro wa uhusiano wa nchi wanachama wa baraza hilo.

Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani (kushoto) na Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudi Arabia

Hivi karibuni, gazeti la Kuwait la Ar-Rai lilizinukuu duru za ngazi ya jauu za kidiplomasia na kuandika kuwa, imepangwa katika kikao kijacho cha wakuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, nchi za Saudi Arabia, Bahrain, Imarati na Misri zifanye suluhu na Qatar.

Mnamo tarehe 5 Juni 2017, nchi hizo nne zilivunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar baada ya kuituhumu kuwa inafadhili ugaidi na kisha zikafungia nchi hiyo mipaka yao ya ardhini, angani na baharini.

Saudia, Bahrain, Imarati na Misri zimeitaka Qatar itekeleze mambo 13 kama masharti ya kufanya nayo na suluhu na maridhiano, lakni serikali ya Doha imekataa kutekeleza matakwa hayo.../

Tags