Serikali mpya ya Mansur Hadi na washirika wasioelewana
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i65307-serikali_mpya_ya_mansur_hadi_na_washirika_wasioelewana
Abdurabbuh Mansur Hadi, Rais aliyejiuzulu wa Yemen, Ijumaa iliyopita alitoa agizo la kuundwa serikali mpya ya nchi hiyo kwa uongozi wa Waziri Mkuu Maeen Abdul-Malik Saeed.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 20, 2020 23:11 UTC
  • Serikali mpya ya Mansur Hadi na washirika wasioelewana

Abdurabbuh Mansur Hadi, Rais aliyejiuzulu wa Yemen, Ijumaa iliyopita alitoa agizo la kuundwa serikali mpya ya nchi hiyo kwa uongozi wa Waziri Mkuu Maeen Abdul-Malik Saeed.

Kuna nukta kadhaa zinazoweza kutathminiwa kuhusiana na serikali hiyo mpya pamoja na agizo la Mansur hadi la kuundwa serikali yenyewe.

Mosi, Mansur Hadi sio Rais halali kwani kipindi chake cha urais wa mpito kilimalizika mwaka 2014. Aidha katika upande mwingine, katika miaka ya hivi karibuni Mansur Hadi amekuwa akiishi uhamishoni huko Riyadh Saudi Arabia na sio Aden yalipo makao makuu ya serikali yake. Si hayo tu, bali ofisi ya Rais Mansurh Hadi imetangaza kuwa, hafla ya kuapishwa serikali mpya haitafanyika Aden. Kuna uwezekano hafla hiyo ikafanyika mjini Riyadh, mahala anapoishi kwa sasa Mansur Hadi. Kwa muktadha huo basi, agizo la kuundwa serikali mpya lililotolewa na kiongozi kama huyu halina mashiko ya kisheria.

Pili, serikali hiyo mpya inaundwa na mawaziri 24 kwa uongozi wa Waziri Mkuu Maeen Abdul-Malik ambayo kwa mujibu wa ripoti, mawaziri 12 wanatoka mikoa ya kaskazini na 12 wengine wanatoka katika maeneo ya kusini mwa Yemen. Aidha mawaziri watano kati ya 12 wanaotoka eneo la kusini ni kutoka Baraza la Mpito la Kusini. Muundo huu unabainisha ukweli huu kwamba, serikali iliyojiuzulu ya Mansur Hadi inachukua mkondo wa kuporomoka siku baada ya siku na nafasi yake huko kusini mwa Yemen imedhoofika sana.

Baraza la Mpito la Kusini

 

Tatu; licha ya kuwa kuundwa serikali hiyo mpya ni katika maazimio ua makubaliano ya Riyadh ya Novemba 2019, lakini moja ya vipengee muhimu vya makubaliano hayo hakijatekelezwa. Kwa mujibu wa hati ya makubaliano ya Riyadh, vikosi vya Baraza la Mpito la Kusini vinapaswa kuunganishwa na Wizara ya Ulinzi. Mansurh Hadi alikuwa akitaka kutekelezwa kipengee cha usalama yaani cha kuunganishwa kwanza vikosi vya Baraza la Mpito la Kusini katika Wizara ya Ulinzi kabla ya kuundwa serikali mpya, ilihali upande wa pili yaani Baraza la Mpito la Kusini lilikuwa likitaka kutekelezwa kwanza kipengee cha kisiasa yaani cha kuundwa serikali mpya kisha ndipo kitekelezwa kipenge cha usalama. Baada ya vuta nikuvute, hatimaye matakwa ya Baraza la Mpito la Kusini yametekelezwa.

Filihali nukta muhimu iliyopo ni hii kwamba, je kipengee cha usalama kinachotaka kuunganishwa na Wizara ya Ulinzi kikosi cha cha Baraza la Mpito la Kusini kitatekelezwa au la? Endapo kipengee hiki hakitatekelezwa na Baraza la Mpito la Kusini mwa Yeme likaendelea kuwa na kikosi chake cha kijeshi, basi kivitendo uundwaji wa serikali hiyo mpya utakabiliwa na mkwamo na hata kusambaratika. Nukta hii imeashiriwa na Muhammad Ali al-Houthi, mjumbe mwandamizi wa Kamati Kuu ya Kisiasa ya Yemen.

 

Katika radiamali yake kuhusu kuundwa serikali mpya ya Mansur Hadi amesema kuwa, katika serikali hii kuna washirika wasioelewana na matokeo yake yatakuwa ni kusambaratika serikali hiyo. Ashirio la Muhammad Ai al-Houthi kuhusiana na washirika wasioelewana linarejea katika hitilafu na mizozo mikubwa iliyopo baina ya serikali iliyojiuzulu ya Mansur Hadi na Baraza la Mpito la Kusini. Katika maafikiano ya Riyadh-2 ya Julai 2020 yaliyotiwa saini huko Riyadh, liliashiriwa suala la kuundwa serikali katika kipindi cha majuma saba, lakini serikali hiyo imeundwa hivi sasa baada ya kupita takribani miezi mitano, ambapo hili lenyewe linabainisha na kuweka wazi kilele cha hitilafu na mivutano mikubwa iliyopo baina ya pande mbili.

Nukta ya nne na ya mwisho ni kwamba, balozi wa Saudia nchini Yemen amesema kuwa, kuundwa serikali hiyo ni mafanikio makubwa kwa wote na akadai kwamba, kuundwa kwa serikali hiyo kwa maafikiano ya kitaifa kutailazimisha Harakati ya Ansarullah ikubaliane na utatuzi wa kisiasa. Baadhi ya mataifa mengine ya Kiarabu yamekaribisha kwa mikono miwili maafikiano hayo.

Pamoja na hayo, kuundwa serikali hiyo ambako kumetimia kwa mashinikizo ya Saudi Arabia kunatia shaka hasa kwa kutilia maanani kwamba, serikali ambayo ndani yake kuna washirika wasioelewana bila shaka haitakuwa na utendaji mzuri na itashindwa na kusambaratika muda si mrefu kama ilivyoshuhudiwa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kwenye serikali ya muungano baina ya Benny Gantz na Benjamin Netanyahu.