Waziri wa Ulinzi wa Yemen: Muungano vamizi wa Saudia umeshindwa
Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amesisitiza kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na utawala wa Saudi Arabia umeshindwa vibaya nchini Yemen na umeangukia pua.
Muhammad Nassir al-Atifi amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya Televisheni ya al-Masirah na kueleza kwamba, muungano wa Saudia na watu wote waliowasaidia wavamizi katika vita dhidi ya Yemen hii leo wamefikia ukingoni na muda si mrefu watajuta kwa hatua yao hiyo.
Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema bayana kwamba, madola vamizi yakiongozwa na Saudia hivi sasa yamo mbioni yakikimbia kutoka nchini Yemen.
Kadhalika Muhammad Nassir al-Atifi amesea kuwa, hii leo uwezo wa kijeshi wa Yemen ni mkubwa mno na kwamba, anatoa bishara njema za ushindi kwa wananchi wa Yemen.

Saudi Arabia huku ikiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa mwezi Mei mwaka 2015 ilianzisha uvamizi wa kijeshidhidi ya nchi maskini ya Kiarabu ya Yemen na kisha kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, angani na nchi kavu.
Vita hivyo vya kidhulma vya Saudi Arabia na waitifaki wake huko Yemen hadi sasa vimesababisha kuuliwa Wayemeni zaidi ya elfu 16, kujeruhiwa makumi ya maelfu na kuwa wakimbizi mamilioni ya wengine. Licha ya jinai zote hizo, lakini hadi sasa Saudia na waitifaki wake wameshindwa kufikia malengo yao.