Kiongozi wa Hamas ataka Saudia iwaachilie huru wafungwa Wapalestina
Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), Ismail Haniya, ameitaka Saudi Arabia iwaachilie huru wafungwa wote Wapalestina inaowashikilia akiwamo afisa wa Hamas.
Akizungumza katika kikao cha kufunga Kongamano la Saba ya Kisiasa la Hamas ambalo lilifanyika kwa njia ya intaneti, Haniya ameikosoa vikali Saudia kwa kuwafunga gerezani Wapalestina kwa sababu tu wanafungamana na Hamas.
Aidha amesema utawala wa kifalme Saudia umekuwa ukiwakamata Wapalestina wengi wanaoishi nchini humo.
Mwezi Machi mahakama moja ya Saudia ilianza kusikiliza kesi ya Wapalestina na Wajordan wapata 68. Wafungwa hao wanakabiliwa na tuhuma bandia za eti kuunga mkono na kufadhili ugaidi pamoja na kuwa wanachama wa 'kundi la kigaidi"
Afisa wa Hamas Dr Mohammed al-Khudari na mwanae, Hani, ni kati ya waliofikishwa kizimbani nchini Saudia.
Al Khudari aliwahi kuwa mwakilishi wa Hamas nchini Saudia kuanzia kati kati ya muongo wa 90 hadi mwaka 2003. Aidha amewahi kushikilia nafasi kadhaa za ngazi za juu katika harakati ya Hamas.
Saudi Arabia imechukua hatua kandamizi dhidi ya harakati ya Hamas na imewakamata wale wote wanaokusanya misaada ya kuwapelekea Wapalestina wanaoishi chini ya mzingiro wa kinyama wa Israel katika Ukanda wa Ghaza.
Hayo yanajiri huku Saudia ikiwa mbioni kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel.