Israel iliharibu nyumba 729 za Wapalestina mwaka 2020
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i65632-israel_iliharibu_nyumba_729_za_wapalestina_mwaka_2020
Utawala haramu wa Israel uliharibu nyumba 729 za raia wa Palestina katika mwaka uliopita wa 2020 kwa kutumia kisingizio cha kujengwa bila ya vibali.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 07, 2021 05:20 UTC
  • Israel iliharibu nyumba 729 za Wapalestina mwaka 2020

Utawala haramu wa Israel uliharibu nyumba 729 za raia wa Palestina katika mwaka uliopita wa 2020 kwa kutumia kisingizio cha kujengwa bila ya vibali.

Katika ripoti yake iliyotolewa jana Jumatano, Kituo cha Haki za Binadamu cha Israel kimesema kuwa Wapalestina 1006 wakiwemo watoto 519 walilazimika kuwa wakimbizi kutokana na bomoa bomoa hiyo ya nyumba na makazi ya raia wa Palestina. Kituo hicho kimesema kuwa, katika mwaka uliomalizika majuzi pia walowezi wa Kizayuni walifanya mashambulizi 248 dhidi ya makazi ya Wapalestina katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi na kwamba mashambulizi hayo yamesababisha hasara kubwa katika nyumba, mashamba na milki za raia hao. 

Wakati huo huo taasisi ya ARIJ imetangaza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umepanga kujenga nyumba mpya 1406 za walowezi katika maeneo yaliyoghusubiwa ya Palestina ya Wadi Asla, Tuhrul Manaf na al Munafis huko kwenye Ukingo wa Magharibi.

Israel inajenga vitongoji vya walowezi katika ardhi ya Palestina

Mwezi uliopita gazeti la Haaretz liliripoti kuwa, Israel imechukua uamuzi wa kuanza kujenga kitongoji kipya kitakachokuwa na maelfu ya nyumba za walowezi huko mashariki mwa Baitul Muqaddas kabla ya kuapishwa rasmi rais mteule wa Marekani, Joe Biden hapo tarehe 20 mwezi huu wa Januari.

Itakumbukwa kuwa azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga marufuku ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.