Katibu Mkuu wa UN: Israel isimamishe haraka ujenzi wa vitongoji
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unapaswa kusimamisha haraka ujenzi wa vitongoji.
Antonio Guterres ametoa sisitizo hilo katika hotuba ya ufunguzi wa kamati ya uchukuaji hatua kwa ajili ya haki zisizokanushika za watu wa Palestina, aliyotoa Alkhamisi kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Amesema ujenzi wa vitongoji unaofanywa na utawala wa Kizayuni katika maeneo unayoyakalia kwa mabavu ndicho kizuizi kikuu cha kupatikana suluhu na amani ya uadilifu na akataka hatua hizo zisitishwe haraka.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, janga la dunia nzima la corona linawaathiri vibaya sana Wapalestina hasa katika Ukanda wa Gaza; na hali ya mfumo wa afya ya jamii katika eneo hilo ni mbaya sana kutokana na ukaliaji ardhi kwa mabavu, hali tete ya kiuchumi pamoja na hali ya kibinadamu na kisiasa katika eneo hilo.
Hatua ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ya kujenga vitongoji vya walowezi katika eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan inakiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Desemba 23, 2016 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio 2334 ambalo liliutaka utawala haramu wa Israel usimamishe haraka na kikamilifu shughuli zote za ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.
Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kwa kuyazayunisha maeneo hayo, kuhakikisha unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.../