May 08, 2021 12:20 UTC
  • Imarati yatakiwa kuangalia upya uhusiano, mapatano yake na Israel

Muungano wa Muqawama Dhidi ya Kuanzishwa Uhusiano na Israel wa Umoja wa Falme za Kiarabu umeitaka serikali ya Imarati, wafanyabiashara na shakhsia huru wa nchi hiyo ya Kiarabu kuangalia upya mapatano ya ushirikiano yaliyofikiwa hivi karibuni baina ya UAE na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tovuti ya habari ya UAE71 imenukuu taarifa ya muungano huo leo Jumamosi ikisema kuwa, matukio yanayoshuhudiwa hivi sasa katika mji mtukufu wa Quds yanaonesha hatari inayowakodolewa macho Wapalestina kwa upande mmoja, na uchu wa Wazayuni wanaotaka kukitokomeza kizazi cha Wapalestina kwa kuwafukuza Baitul Muqaddas na kuwahamishia Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na maeneo mengine wanaoyakaliwa kwa mabavu kwa upande wa pili.

Taarifa ya Muungano wa Muqawama Dhidi ya Kuanzishwa Uhusiano na Israel wa Umoja wa Falme za Kiarabu kadhalika imeitaka Imarati isitishe mara moja uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara ilioanzisha na utawala haramu wa Israel.

Imebainisha kuwa, Quds ni mji mkuu wa milele wa Palestina, na kwamba Palestina itabakia daima kuwa taifa la Kiislamu na Kiarabu. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, Imarati kama taifa jingine la Kiislamu na Kiarabu ina wajibu wa kuwahami, kuwatetea na kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina.

Katika miezi mitatu ya mwisho wa mwaka uliomalizika wa 2020, nchi nne za Kiarabu za Imarati, Bahrain, Sudan na Morocco zilianzisha uhusiano rasmi na utawala haramu wa Kizayuni na Israel.

Hatua hiyo ya kihaini na ya usaliti iliyofanywa na nchi hizo ambayo ni kushiriki kwenye mpango wa mapatano wa Kimarekani na Kizayuni, imelaaniwa na kukosolewa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Tags