Malengo ya Israel ya kufanya luteka ya kijeshi ya mwezi mzima
Tangu juzi Jumapili tarehe 9 Mei, jeshi la utawala wa Kizayuni limeanzisha luteka na mazoezi maalumu ya kijeshi yatakayodumu kwa muda wa mwezi mmoja.
Manuva makubwa ya kijeshi ya Israel ambayo hayajawahi kutokea mfano wake katika kipindi cha miaka mingi iliyopita, yameanza katika hali ambayo, kwa upande mmoja Benjamin Netanyahu ameshindwa kuunda serikali, huku utawala pandikizi wa Israel ukiwa ndani ya mkwamo mkubwa ambao haujawahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni; na kwa upande wa pili, tangu mwezi Mei mwaka huu hadi hivi sasa, kila siku ya Jumamosi, wakazi wa utawala wa Kizayuni wanafanya maandamano ya kulalamikia matatizo ya kiuchumi. Kwa kuzingatia hali hiyo, wataalamu wa mambo wanajiuliza, ni ipi sababu ya viongozi wa utawala wa Kizayuni ya kuamua kufanya luteka na mazoezi makubwa na ya muda mrefu kiasi chote hicho ya kijeshi?
Wakuu wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni wanadai kuwa lengo kuu la luteka hiyo ya muda mrefu ni kuwaandaa wanajeshi wa Israel kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi yanayoweza kufanywa na makundi ya muqawama katika eneo hili. Kanali ya 13 ya Israel imewanukuu wakuu wa kijeshi wa utawala huo wakisema kuwa, moja ya malengo makuu ya mazoezi hayo ya kijeshi ni kukabiliana na mashambulizi makubwa ya makombora kutoka katika mipaka ya kusini, kaskazini na mashariki kwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.
Ukweli ni kuwa, manuva hayo ya kijehsi ya Israel yana uhusiano wa moja kwa moja na hali ya hivi sasa ya Ukanda wa Ghaza na Quds. Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wamekumbwa na upinzani mkali kutoka kwa wananchi wa Palestina wa mji wa Baytul Muqaddas. Mapigano makali yamezuka baina ya pande mbili kiasi kwamba katika kipindi cha siku tatu zilizopita, zaidi ya Wapaletina 300 wamejeruhiwa na wanajeshi makatili wa utawala wa Kizayuni. Uhakika ni kuwa Israel hivi sasa inaogopa mapigano hayo yasije yakaishia kwenye operesheni na mashambulizi ya makombora kutoka kwa makundi ya muqawama ya Palestina ya Ukanda wa Ghaza. Woga huo umebainishwa wazi na vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni. Gazeti la Israel Hayom limeandika, changamoto kubwa liliyo nayo jeshi la Israel hivi sasa ni kuzuia kubadilika operesheni za mtu mmoja mmoja na kuwa mapigano na vita vikubwa vya pande zote.
Zaidi ya hayo, mazoezi hayo makubwa na ya muda mrefu zaidi ya kijeshi ya Israel yameanza baada ya matukio ya kiusalama ya wiki tatu zilizopita katika ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel. Tarehe 21 mwezi uliopita wa Aprili kulitokea mripuko katika taasisi za makombora za Israel, siku iliyofuata kukafanyisha shambulio la kombora lililotua karibu na taasisi ya nyuklia ya Dimona ya utawala wa Kizayuni; kombora hilo lilivuka kilomita nyingi ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni bila ya mfumo wa kujikinga na makombora wa utawala huo pandikizi, kuliona kombora hilo hadi lilipopiga palipokusudiwa. Yote hayo yameonesha kiwango cha juu mno cha udhaifu wa kiulinzi wa Israel licha ya majigambo yake makubwa ya eti jeshi lake halishindiki. Vile vile kushindwa siasa za kiuadui za Marekani ambayo ni muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni, za kujaribu kuipigisha magoti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia mashinikizo ya kiwango cha juu kupindukia, ni sababu nyingine ya kufeli vibaya mabeberu wa dunia, kisiasa na kijeshi. Kabla ya hapo vyombo vya usalama wa Israel vilionya kuhusu udhaifu wa utawala huo wa kukabiliana na mashambulizi kutoka kaskazini na kusini mwa ardhi za Palestina zilizobadilishwa jina na wavamizi hao na kuitwa Israel. Duru hizo za kiusalama zilisema, zina wasiwasi mkubwa kwamba Israel haina uwezo wa kukabiliana na mashambulizi ya kila upande ya makombora
Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana wataalamu wa mambo wakasema kuwa, kufanyika wakati huu mazoezi na luteka ya muda mrefu kiasi chote hicho ya kijeshi ya Israel, kabla ya jambo lolote, ni uthibitisho wa woga na hofu kubwa waliyo nayo Wazayuni kuhusu usalama wa dola lao pandikizi.