Maafisa usalama wa Misri wawasili katika Ukanda wa Ghaza, Palestina
(last modified Sat, 29 May 2021 09:40:32 GMT )
May 29, 2021 09:40 UTC
  • Maafisa usalama wa Misri wawasili katika Ukanda wa Ghaza, Palestina

Duru za habari zimetangaza kuwa ujumbe maalumu wa maafisa usalama wa Misri umewasili katika Ukanda wa Ghaza huko Palestina kwa ajili ya kufanya mazungumzo na wakuu wa makundi ya muqawama.

Falastin al Yaum imeripoti leo Jumamosi kwamba, maafisa wa shirika la kijasusi la Misri wakiongozwa na Ahmad Abdul Khaliq anayehusika na kadhia ya Palestina wamewasili katika Ukanda wa Ghaza huko Palestina ikiwa ni mara ya tatu tangu yalipofikia makubaliano ya kusitisha vita kati ya wanamuqawama wa Palestina na utawala wa Kizayuni zaidi ya wiki moja iliyopita.

Miongoni mwa viongozi wa Palestina watakaoonana na ujumbe huo wa Misri ni Marwan Isa, kiongozi mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya Naibu Kamanda Mkuu wa Brigedi za Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS.

Israel imefanya jinai kubwa kupindukia dhidi ya wananchi wa Ghaza na makazi yao huko Palestina

 

Taarifa zinasema kuwa Misri imewajulisha viongozi wa HAMAS kwamba mazungumzo yatakayofuatia lazima yajumuishe suala la kuachiliwa huru mateka. Cairo imesema, utawala wa Kizayuni unalipa umuhimu mkubwa mno suala hilo na unaliunganisha na kadhia nzima ya kusimamishwa vita na kujengwa upya Ukanda wa Ghaza.

Duru za Misri zimetangaza pia kuwa, lengo jingine la safari ya ujumbe huo wa maafisa wake usalama huko Ghaza ni kuandaa mazingira ya kuingia kwenye eneo hilo Abbas Kamil, mkuu wa shirika la kijasusi la Misri. Mbali na Ghaza, Abbas Kamil anatarajiwa kutembela pia Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Kuanzia tarehe 10 mwezi huu wa Mei utawala wa Kizayuni wa Israel ulifanya mashambulizi makubwa ya pande zote dhidi ya Ukanda wa Ghaza huko Palestina kwa muda wa siku 12 na kufanya uharibifu mkubwa sambamba na kuua na kujeruhi idadi kubwa ya Wapalestina wasio na hatia.

Tags