Misri yauonya utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu Ukanda wa Ghaza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, usiku wa kuamkia leo ameuonya utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu hatari za kuvunja makubaliano ya kusimamisha vita ya Ghaza.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, onyo hilo limetolewa katika mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry na Gabi Ashkenazi, waziri wa mambo ya nje wa Israel.
Wakati huo huo Abbas Kamil, Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Misri ameelekea Tel Aviv na Ramallah, sambamba na safari ya waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni mjini Cairo. Hiyo ni ziara ya kwanza ya waziri wa mambo ya nje wa Israel huko Misri tangu mwaka 2008.
Juzi Jumamosi, Falastin al Yaum iliripoti kwamba, maafisa wa shirika la kijasusi la Misri wakiongozwa na Ahmad Abdul Khaliq anayehusika na kadhia ya Palestina wamewasili katika Ukanda wa Ghaza ikiwa ni mara ya tatu tangu yalipofikia makubaliano ya kusitisha vita kati ya wanamuqawama wa Palestina na utawala wa Kizayuni zaidi ya wiki moja iliyopita.
Miongoni mwa viongozi wa Palestina walioonana na ujumbe huo wa Misri ni Marwan Isa, kiongozi mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa na Naibu Kamanda Mkuu wa Brigedi za Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS.
Duru za Misri zilitangaza pia kuwa, lengo jingine la safari ya ujumbe huo wa maafisa wake usalama huko Ghaza ni kuandaa mazingira ya kuingia kwenye eneo hilo Abbas Kamil, mkuu wa shirika la kijasusi la Misri. Zilisema, mbali na Ghaza, Abbas Kamil atatembelea Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kuanzia tarehe 10 mwezi huu wa Mei utawala wa Kizayuni wa Israel ulifanya mashambulizi makubwa ya pande zote dhidi ya Ukanda wa Ghaza huko Palestina kwa muda wa siku 12 na kufanya uharibifu mkubwa sambamba na kuua na kujeruhi idadi kubwa ya Wapalestina wasio na hatia.