HAMAS: Umma wa Kiislamu unapaswa kuungana kukomesha ugaidi wa Israel + Video
(last modified Thu, 10 Jun 2021 06:52:32 GMT )
Jun 10, 2021 06:52 UTC
  • HAMAS: Umma wa Kiislamu unapaswa kuungana kukomesha ugaidi wa Israel + Video

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, Umma wa Kiislamu una jukumu la kuungana na kuwa kitu kimoja kama unataka kweli kukikomboa Kibla chao cha Kwanza yaani Msikiti wa al Aqsa na kukomesha jinai na ugaidi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hazem Qassem alisema hayo jana na kuongeza kuwa, utawala wa Kizayuni unayavunjia heshima mara kwa mara matukufu ya Waislamu huko Palestina na hadi hivi sasa unaendelea kufanya jinai na kuwachochea Waislamu na Waarabu.

Ameongeza kuwa, kitendo cha jana cha Israel cha kushambulia ardhi ya Syria ni uvamizi na ni jinai mpya ya kinyama na ya wazi. Hata hivyo amesema, hizo ndizo siasa kuu za utawala wa Kizayuni zilizosimama juu ya uvamizi na kupora mali na ardhi za mataifa mengine.

Mapema jana asubuhi, duru za Syria zilirusha hewani mkanda wa video unaaonesha jinsi jeshi la nchi hiyo linavyokabiliana na mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni kwenye mji mkuu Damascus.

Shirika rasmi la habari la Syria SANA limethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, mfumo wa kujilinda na makombora wa nchi hiyo umefanikiwa kutungua makombora mengi yaliyovurumishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye anga ya Damascus.

Baada ya kuchezea kipigo katika uvamizi wake wa siku 12 kwenye Ukanda wa Ghaza hivi karibuni, utawala wa Kizayuni unafanya njama mbalimbali za kuonesha kuwa una nguvu na unaweza kufanya lolote bila ya kujali kitu chochote. Hata hivyo, Israel imezidi kuaibika baada ya kushindwa kukabiliana na vipigo vya makombora na maroketi kutoka kwa wanamapambano wa Palestina wa Ukanda wa Ghaza ambao licha ya kuzingirwa kila upande kwa miaka mingi na Wazayuni, lakini Wapalesitna hao wanazidi kuwa imara siku baada ya siku.

Tags