Makundi ya muqawama ya Iraq: Tutalipiza kisasi dhidi ya Marekani
Makundi ya muqawama ya Iraq yametangaza kuwa, yatalipiza kisasi mashambulizi ya Marekani dhidi ya ngome za kundi la Hashdu Shaabi.
Makundi ya muqawama ya Iraq leo Jumatatu yametoa taarifa ya pamoja katika radiamali yao kwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya ngome za Hashdu Shaabi katika mpaka wa Syria na Iraq na kueleza kuwa: 'Sisi hatutakaa kimya mkabala na kuendelea kuwepo wanajeshi vamizi wa Marekani nchini; hatua inayokinzana na katiba, uamuzi wa bunge na matakwa ya wananchi wa Iraq.'
Makundi ya muqawama ya Iraq yamesema kuwa, vikosi vamizi vya Marekani vingali vinaendeleza jinai zao huko Iraq kwa kuwashambulia wanamuqawama wa harakati ya Hashdu Shaabi na kusisitiza kuwa, watalipiza kisasi cha damu za mashahidi wa mashambulizi hayo na kuwa adui ataonja ladha chungu ya kisasi hicho.
Kundi la muqawama la Kataeb Sayyid Shuhada la Iraq pia awali lilitangaza kuwa, kuanzia sasa vita baina yao na wanajeshi vamizi wa Marekani havitakuwa na mipaka; na kwamba hatua ya kwanza ya vita hivyo ni kuzishambulia ndege za wanajeshi hao vamizi katika anga ya Iraq.
Vyombo vya habari huko Iraq na Syria leo asubuhi vimetangaza habari ya kujiri mashambulizi ya anga ya marekani katika ngome za kundi la Hashdu Shaabi katika eneo la Bukamal katika mpaka wa Syria na Iraq. Wanamuqawama wanne wa Hashdu Shaabi wameuliwa shahidi na watatu wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo.