Malengo ya Iraq katika kuandaa kikao cha nchi jirani
Serikali ya Iraq inafanya juhudi za kuandaa kikao cha viongozi wa nchi za eneo na nchi kadhaa za kimataifa kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti.
Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq tayari amewaalika rasmi viongozi wa nchi za Iran, Uturuki, Saudi Arabia, Kuwait, Misri na Jordan kushiriki kikao hicho cha Baghdad. Baadhi ya vyanzo vya habari vinasema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa viongozi wa nchi kadhaa za Ulaya akiwemo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kualikwa katika kikao hicho.
Al-Kadhimi ambaye anashikilia kiti cha waziri mkuu wa Iraq tokea mwezi Mei mwaka uliopita wa 2020 ameelekeza juhudi zake kubwa katika siasa za nje. Kufikia sasa amefanya vikao kadhaa vya pande tatu na nchi za Jordan na Misri, ambapo mwezi juni uliopita alikutana mjini Baghdad na Rais Abdulfattah as-Sisi wa Misri na Mfalme Abdallah wa Pili wa Jordan.
Mbali na hayo, serikali ya Iraq imekuwa ikifanya upatanishi kati ya serikali za Iran na Saudi Arabia ambapo kufikia sasa imefanya vikao vitatu na maafisa wa nchi mbili hizi katika uwanja huo, vikao ambavyo vimeakisiwa sana na vyombo vya habari vya kieneo na kimataifa.
Kikao cha nchi jirani ambacho kimepangwa kufanyika kwa uenyeji wa serikali ya Baghdad mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti kwa hakika ni duru ya tatu ya juhudi zinazofanywa na serikali ya al-Kadhimi katika uwanja wa siasa za kieneo na inatazamiwa kuwa mara hii nchi kadhaa muhimu za kimataifa zitashiriki katika kikao hicho. Hata kama serikali ya Iraq imewaalika Mfalme Salman wa Saudia, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kushiriki kikao cha Baghdad lakini hadi sasa haijulikani vizuri nchi tatu hizo muhimu katika eneo zitatuma wawakilishi wao katika kikao hicho kwa kiwango gani.
Kuna mitazamo miwili tofauti kuhusu kufanyika vikao vya namna hiyo katika eneo. Baadhi ya wachambuzi wanasema al-Kadhimi anataka kutumia vikao hivyo kuimarisha nafasi ya Baghdad katika eneo, kutatua matatizo yaliyopo kati ya nchi yake na baadhi ya nchi za eneo na hatimaye kuinufaisha kiuchumi serikali ya Iraq. Wanaounga mkono vikao hivyo wanaamini kuwa vitaimarisha mahusiano ya Iraq na nchi jirani na kupunguza changamoto zinazoikabili.
Katika uwanja huo, Aamir al-Faiz, mwachama wa Kamisheni ya Mahusiano ya Kigeni ya Bunge la Iraq anasema: 'Baghdad inafanya juhudi za kuimarisha nafasi yake katika eneo.'
Adel al-Ashram, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Iraq pia anaamini kwamba Iraq inahitaji sana kuwa na uhusiano mzuri na nchi jirani na za kieneo na kwamba jambo hilo litaisaidia pakubwa katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama.
Mtazamo mwingine ni kwamba vikao hivyo havitakuwa na matunda yoyote kwa taifa la Iraq bali vinalenga tu kuimarisha nafasi ya kisiasa ya Mustafa al-Kadhimi na waungaji mkono wake katika muundo wa madaraka ya nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo Iraq inahitajia zaidi wawekezaji wa kigeni na msaada wa kiuchumi kuliko nchi nyingine yoyote ile ya eneo.
Katika uwanja huo, Makki an-Nizal, mchambuzi wa Iraq anasema kwamba vikao hivyo ni vya kimaonyesho tu na kwamba uzoefu wa vikao vingine kama hivyo huko nyuma unathibitisha wazi kuwa washiriki husahau kila kitu na kutoinufaisha Iraq kwa lolote lile mara tu baada ya kutoka kwenye kumbi za vikao hivyo. Anasema baadhi ya watu wanataka kutumia vikao hivyo ili kuendelea kumbakisha madarakani al-Kadhimi.
Mtazamo huu una umuhimu mkubwa kwa kutilia maanani kwamba uchaguzi wa mapema wa bunge la Iraq umepangwa kufanyika mwezi Oktoba ujao na bila shaka al-Kadhimi ana nafasi nzuri zaidi ya kushinda uchaguzi huo kuliko washindani wake wengine wa kisiasa.