Muqtada al-Sadr: Mkutano wa Baghdad umeonesha umuhimu wa Iraq
Kiongozi wa Harakati ya Al-Sadr ya nchini Iraq amesema Mkutano wa Baghdad uliofanyika juzi Jumamosi umeonesha nafasi na umuhimu wa Iraq katika eneo la Asia Magharibi.
Sayyid Muqtada al-Sadr amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter jana Jumapili na kuongeza kuwa, "Nukta ya kuvutia zaidi katika kikao hicho ni kufunguka kisiasa Iraq katika uga wa kieneo na kimataifa, sambamba na kuzikaribisha nchi za Kiarabu."
Iran, Saudi Arabia, Uturuki, Kuwait, Imarati, Jordan, Misri na Qatar zimeshiriki katika mkutano huo wa Baghdad. Aidha nchi 5 wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimewakilishwa katika mkutano huo, huku Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa akishiriki yeye binafsi.
Sayyid Muqtada al-Sadr amesema bayana kuwa: Mkutano wa Baghdad umekuwa wa kidugu zaidi hata kabla haujawa wa kisiasa au kitu kingine, na kwa msingi huo adui katu hawezi kuufuta ama kwa maneno au vitendo.
Kiongozi huyo wa kidini nchini Iraq amesisitiza kuwa, imekuwa sahali kuuandaa mkutano huo nchini Iraq, jambo ambalo lina umuhimu mkubwa wa kisiasa na kiuchumi kwa taifa hilo la Kiarabu; na hilo linaonesha umuhimu wa Iraq katika eneo na vile umuhimu wa mamlaka ya kujitawala.
Washiriki wa kongamano hilo wamepongeza jitihada za taifa la Iraq katika kupambana na ugaidi huku zikisisitizia haja ya kukabiliana na aina zote za ugaidi.