Hujuma ya kigaidi ya Kunduz, na majukumu ya kundi la Taliban
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i75574-hujuma_ya_kigaidi_ya_kunduz_na_majukumu_ya_kundi_la_taliban
Waislamu wasiopungua mia moja wameuawa katika shambulizi la kigaidi lililolenga waumini waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala ya Ijumaa wiki hii katika mji wa Kunduz nchini Afghanistan na wengine karibu mia mbili wamejeruhiwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 10, 2021 02:26 UTC
  • Hujuma ya kigaidi ya Kunduz, na majukumu ya kundi la Taliban

Waislamu wasiopungua mia moja wameuawa katika shambulizi la kigaidi lililolenga waumini waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala ya Ijumaa wiki hii katika mji wa Kunduz nchini Afghanistan na wengine karibu mia mbili wamejeruhiwa.

Shambulizi hilo limelenga msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika eneo la Khan Abad na tayari kundi la Daesh la ISIL-K limetangaza kuwa ndilo lililohusika na hujuma hiyo.

Shambulizi hilo limefanyika baada ya kundi la Taliban kudai kuwa, kundi la Daesh si tishio kubwa kwa Taliban na kwamba litaangamizwa hivi karibuni nchini Afghanistan. Tawi la kundi la Daesh la ISIL-K limezidisha hujuma na mashambulizi dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Afghanistan katika wiki za karibuni. 

Tawi la kundi la Daesh la ISIL-K  

Shambulizi hilo linatajwa kuwa baya zaidi nchini Afghanistan tangu kundi la Taliban liliposhika tena madaraka ya nchi hiyo mwezi Agosti mwaka huu. Taasisi na makundi mbalimbali za kikanda na kimataifa yamelaani vikali hujuma hiyo ya kigaidi. 

Katibu Mkuu wa umoja huo, Antonio Guterres amelaani vikali shambulizi la kigaidi lililolenga msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mkoa wa Kunduz nchini Afghanistan. Guterres pia ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa hujuma hiyo ya kigaidi na kuwatakia shifaa watu waliojeruhiwa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amelaani vikali hujuma hiyo na kusema Jamhuri ya Kiislamu inalaani ugaidi katika sura zake zote na magaidi wote. 

Japokuwa kundi hilo la kigaidi si tishio kwa Taliban lakini linahesabiwa kuwa hatari na tishio kubwa kwa watu wa Afghanistan hususan wafuasi wa madhehebu na kaumu za waliowachache. Kundi hilo linafanya harakati zake kwa shabaha ya kuibua na kuchochea vita na mapigano ya kimadhehebu na kikaumu. 

Maulawi Naeemul Haq Haqani ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Afghanistan anasema: Kundi la kigaidi la Daesh ni mtoto wa kigeni ambaye anaendesha shughuli zake nchini Afghanistan kwa shabaha ya kuzusha matatizo kwa wananchi. Kundi hili linatumiwa kwa ajili ya kuibua migawanyiko na fitina baina ya Waafghani.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kwa kutilia maanani kuwa baadhi ya wanachama wa Taliban wanapinga sera za kufanya suluhu na mapatano na Marekani yumkini kwamba, suala hilo ni miongoni mwa sababu za hujuma na machafuko yanayojiri sasa huko Afghanistan. Kwa msingi huo kundi la Taliban linawajihiana na hali ngumu sana kwa ajili ya kudhamini usalama na amani ya watu wa Afghanistan. Hii ni kwa sababu wapinzani wa kundi hilo wakiwemo maafisa wa upelelezi na ujasusi wa serikali iiyoondoka madarakani ya Muhammad Ashraf Ghani, wanaweza kutekeleza mashambulizi kama haya kwa nia ya kulitia doa kundi hilo na kuonesha udhaifu wake katika masuala ya utawala na kulinda usalama.

Rais Ashraf-Ghani wa Afghanistan aliyekimbiai nchi 

Alaa kulli hal, kundi la Taliban linaloshika hatamu za kuongoza Afghanistan, lina jukumu zito la kulinda usalama na amani ya nchi hiyo hususan jamii za waliowachache kimadhehebu na kikaumu. Hivyo iwapo litashindwa kudhamini usalama na kukabiliana na makundi ya kigaidi kama lile la ISIL-K, litakabiliwa na matatizo makubwa sana katika siku za usoni. Hasa ikitiliwa maanani kwamba, jamii ya kimataifa inafuatilia kwa makini yanayojiri Afghanistan baada ya kundi hilo kushika tena madaraka ya nchi kufuatia miaka 20 ya uvamizi wa Marekani na washirika wake.