25 wauawa katika mashambulizi pacha ya mabomu Afghanistan
Makumi ya watu wameuawa katika milipuko miwili ya mabomu iliyotokea leo katika hospitali ya kijeshi katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.
Qari Saeed Khosty, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan amesema mbali na watu 25 kuuawa katika milipuko hiyo iliyopishana kwa sekunde kadhaa, wengine zaidi ya 50 wamejeruhiwa.
Milipuko hiyo imelenga Hospitali ya Sardar Mohammad Daud Khan yenye vitanda 400, katika eneo la Wazir Akbar Khan, katikati mwa Kabul. Hospitali hiyo ndiyo taasisi kubwa zaidi ya matibabu ya jeshi la Afghanistan.
Habari zaidi zinasema kuwa, baada ya kujiri milipuko hiyo, milio ya risasi ilirindima ndani na nje ya hospitali hiyo na kuibua taharuki. Hospitali hiyo lilikabiliwa na shambulio la kigaidi mwaka 2017, ambapo magaidi waliojifanya kuwa wahudumu wa afya waliua watu 30 kwa kuwamininia risasi.
Hakuna kundi lililotangaza kuhusika na mashambulio hayo ya leo Jumanne, ingawaje shirika la habari la Bakhtar limeripoti kuwa, wanachama kadhaa wa kundi la kigaidi la ISIS walioneka wakiingia hospitalini hapo na kukabiliana vikali na maafisa usalama.
Mwezi uliopita, kundi hilo la ukufurishaji lilitangaza kuhusika katika hujuma za kigaidi dhidi ya misikiti ya Waislamu wa madhehebu ya Shia huko Kunduz na Kandahar wakati wa Sala ya Ijumaa katika muda wa wiki mbili mfululizo.