Dalili za kupungua nafasi ya Marekani Asia Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i76582-dalili_za_kupungua_nafasi_ya_marekani_asia_magharibi
Tarehe 4 Novemba imetengwa katika kalenda ya Iran kuwa siku ya mapambano dhidi ya uistikabari wa dunia (ubeberu/ujeuri)
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 06, 2021 03:26 UTC
  • Dalili za kupungua nafasi ya Marekani Asia Magharibi

Tarehe 4 Novemba imetengwa katika kalenda ya Iran kuwa siku ya mapambano dhidi ya uistikabari wa dunia (ubeberu/ujeuri)

Sababu ya siku hii kupewa jina hilo inatokana na matukio ya mapambano dhidi ya Marekani katika historia ya sasa ya Iran. Baada ya kupita miaka 43 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran hivi sasa dalili za kudhoofika na kupungua nafasi ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi zinaonekana wazi kuliko wakati mwingine wowote. Iran ndiyo nchi iliyo katika mstari wa mbele zaidi katika mapambano dhidi ya ubeberu wa Marekani kuliko nchi nyingine yoyote ile duniani.

Moja ya sababu za kupungua nafasi ya Marekani Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) ni kujiunga na kudhamini nchi nhiyo makundi ya kigaidi kwa ajili ya kufikia malengo yake haramu katika eneo. Marekani ambayo imekuwa ikijinadi kuwa mbeba bendera ya mapambano dhidi ya ugaidi kimataifa sasa yenyewe imejiunga na makundi hatari ya kigaidi ili kuendeleza siasa zake kieneo na hasa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mfano wa wazi zaidi katika uwanja huo ni mauaji ya kigaidi iliyoyatekeleza dhidi ya Luteni Jenerali Haj Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Kamanda wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq (Hashd al Shaabi) karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, mji mkuu wa Iraq.

Droni ya kisasa ya Marekani Global Hawk

Dalili nyingine inayothibitisha kupungua nafasi ya Marekani Asia Magharibi ni kutunguliwa ndege ya kisasa isiyo na rubani ya nchi hiyo na jeshi shupavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tarehe 20 Juni 2019 Jeshi la Iran halikusita katika kuchukua uamuzi wa kutungua ndege hiyo isiyo na rubani (droni) aina ya Global Hawk mara tu baada ya kukiuka anga ya Iran, na hii ni katika hali ambayo ndege hiyo ilichukuliwa kuwa ya kisasa kabisa ambayo haingeweza kuonekana kirahisi angani wala kutunguliwa.

Kutunguliwa ndege hiyo na jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kulithibitisha wazi kuwa nguvu ya kijeshi ya Marekani haiogepewi tena kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Hatua nyingine ya kijasiri iliyochukuliwa na jeshi shupavu la Iran katika kushambulia kwa makombora kituo cha kijeshi cha Marekani huko Ain al-Asad nchini Iraq ni dalili nyingine inayothibitisha kuwa hatua za kichokozi na kigaidi za Marekani Asia Magharibi na hasa dhidi ya Iran hazitaachwa bila kujibiwa. Hiyo ni dalili nyingine inayothibitisha kuwa nafasi ya Marekani Asia Magharibi inapungua kwa kasi.

Kupungua huko kwa nafasi ya Marekani katika eneo, kulidhihirika wazi kufuatia uamuazi wa nchi hiyo wa kuondoa haraka na kwa fedheha wanajeshi wake vamizi nchini Afghanistan na sasa huko Iraq. Tukiachilia mbali madhara yaliyosababishwa na uwepo wa miongo miwili wa askari hao wa kigeni huko Afghanistan, ni wazi kuwa uamuzi wa Washington wa kuwarejesha nyumbani tena kwa fedheha askari hao ulitokana na Marekani kutambua wazi kuwa nafasi yake ya kijeshi katika nchi za Asia Magharibi inaendelea kupungua kwa kasi na kwamba kuendelea uwepo wake katika eneo kunazidisha tu chuki dhidi ya Wamarekani.

Ni kwa msingi huo ndipo watawala wa Washington wakaamua pia kuondoa askari wao huko Iraq ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Ni wazi kuwa Marekani imefikia natija kwamba kuendelea uwepo wake wa kijeshi katika eneo la Asia Magharibi si tu hauiongezei nchi hiyo nguvu yoyote bali unadhuru nafasi na maslahi yake katika mfumo wa dunia, kwa sababu kuendelea kupingwa siasa za Marekani kunaweza kuchukuliwa kuwa mfano wa kufuatwa na nchi nyingi kimataifa.

Tukio la karibuni la jeshi la Iran kuifedhehesha Marekani katika maji ya Bahari ya Oman

Muhammad Ali Ranjbar, mtaalamu wa masuala ya Marekani anasema kuhusiana na kupungua nafasi ya Marekani katika eneo muhimu la Asia Magharibi kwamba: 'Picha za kuaibisha na kufedhehesha za kuondoka Wamarekani huko Afghanistan, kushambuliwa kituo cha kijeshi cha Ain al-Asad na kutunguliwa ndege isiyo na rubani ya Global Hawk, yote hayo ni mambo yanayothibitisha wazi uongo na propaganda kwamba Marekani ni nchi yenye nguvu kubwa isiyoweza kushindwa duniani. Leo dhana hii imepata nguvu kuwa, eneo la Asia Magharibi litakuwa eneo bora lenye amani na utulivu bila ya uwepo wa Marekani.'